Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wazuru Daraja jipya la Wami, watoa maelekezo

Daraja La Wami 780x470.jpeg Wabunge wazuru Daraja jipya la Wami, watoa maelekezo

Mon, 14 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya miundombinu imetoa wito kwa wananchi kulitunza Daraja jipya la Wami (m 513.5) na barabara zake unganishi (km 3.8), ili liweze kudumu kwa muda mrefu.

Hayo yamesemwa mkoani Pwani na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, mara baada ya wajumbe wa kamati hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo na barabara zake ambapo wameridhishwa na kazi zilizofanyika mpaka sasa na kusema kuwa kuwa uwepo wa daraja hilo utakidhi ongezeko la magari yanayopita katika daraja hilo kulinganisha na daraja la zamani.

“ … Kumekuwa na tabia ya kuharibu sana miundombinu ambayo imewekezwa na Serikali pindi inapokamilika wakati miradi hii yote ni mali ya wananchi hivyo muilinde, muitunze kwa kuwa ina manufaa makubwa sana kwa wananchi na Taifa”, amesisitiza Kakoso.

Aidha, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya miundombinu imeipongeza Serikali kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 75 katika utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo ambalo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 97 na tayari wananchi wameanza kunufaika na miundombinu hiyo.

“Kamati inamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa za kuleta maendeleo kwa wananchi ambapo ametoa fedha kwa ujenzi wa daraja jipya la wami ambalo kwa kiwango kikubwa sana litawasaidia wananchi na kuepusha ajali zilizokuwa zikitokea mara kwa mara huko nyuma”, amesema Mwenyekiti huyo.

Kamati hiyo imeshauri Wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Pwani kutunza na kuweka na mazingira wezeshi na salama katika daraja hilo kwa kupanda nyasi na miti ili kulifanya daraja hilo liwe endelevu na kutunza uoto wa asili.

Pia imeagiza Wizara ya Ujenzi kutenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho makubwa Daraja la zamani la Wami ili kuongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi na kurahisisha shughuli zao kipindi chote na majira yote.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, ameishukuru Kamati kwa kukagua na kujiridhisha na mradi huo na kuiahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo.

Eng. Kasekenya ameeleza kukamilika kwa Daraja jipya la Wami kutasaidia kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwani utapunguza muda wa safari pamoja na ajali zilizokuwa zikitokea mara kwa mara katika daraja la zamani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live