Ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Serikali ilipositisha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo ameziomba taasisi za fedha kupunguza riba za mikopo ili kuwasaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
April 13, 2023 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kusitishwa kwa utoaji wa mikopo hiyo na wakati akihitimisha Hoja yake ya Makadilio ya Maombi na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2023/24 bungeni Dodoma, kufuatia taarifa za kuwepo kwa ufujaji wa fedha hizo.
Akizungumza leo Mei 8, 2023 na wanawake wajasiriamali ambao ni wanufaika wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Amenye group kilichopo jijini hapa, Fyandomo amesema wakati Serikali ikiwa imesitisha mikopo hiyo, watapeleka ombi kwa taasisi za fedha kulegeza masharti kwa wakopaji.
“Uamuzi huo wa Serikali kuelekeza mikopo hiyo kwenye taasisi za kifedha utasaidia kurejesha nidhamu na matumizi sahihi ya mikopo, lakini suala kubwa ni kuomba taasisi hizo kutoweka riba kubwa za mikopo.
“Asilimia kubwa wakopaji wa mikopo ni wale walikuwa wakinufaika kwenye halmashauri zetu ambao ni vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu sasa tuone kwa pamoja namna gani ya kuwavutia kukopa kama hapo awali,” ameseme Fyandomo.
Kwa upande wake Mbunge Viti Maalum Zanzibar, Mariam Mwinyi amesema Serikali ina lengo zuri la kuona kunakuwa na mifumo rafiki ya utoaji wa mikopo ambayo itaingia kwenye mzunguko na kunufaika makundi mengi zaidi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Serikali yetu ni sikivu tuna imani kubwa mikopo hiyo itawanufaisha ikiwepo sisi kama wabunge kushawisha Serikali kuzungumza na taasisi za mabenki kuangalia suala zima la riba nafuu ya mikopo kwa makundi hayo,” amesema.
Mwenyekiti wa kikundi hicho Amenye David, amesema walilazimika kuanzisha kikundi kwa lengo la kuinuana kiuchumi ili kuwezesha wanawake kumudu kuendesha maisha ya kila siku na kuhudumia familia ikiwepo kusomesha .