Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waathirika mafuriko Kilosa wapatiwa misaada ya Sh50 milioni

Kilosa Mhm.jpeg Waathirika mafuriko Kilosa wapatiwa misaada ya Sh50 milioni

Wed, 13 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waathirika wa mafuriko Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wamepatiwa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 50 kwa lengo la kuwasaidia walioathirika zaidi na mafuriko hayo ili waweze kujikimu kimaisha wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya kina.

Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka, Disemba 12, 2023, Mkuu wa Mkoa huo Adam Kighoma Malima amesema wananchi zaidi ya 4700 wameathiriwa na mafuriko hayo huku nyumba 997 zilizingirwa na maji kati ya hizo nyumba 85 zimesombwa na maji kabisa.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo madaraja manne, Barabara na mashamba vyakula na mali nyingine huku watu wawili wakiripotiwa kufariki kutokana mafuriko hayo.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amerudia maelekezo aliyoyatoa hivi karibuni kwa wananchi wa kilosa kutodharau ushauri wa wataalam wa kutorudi kwenye nyumba zao bila kujiridhisha kwa wataalam hao hususan zilizothiriwa sana na mafuriko huku akibainisha kuwa nyumba hizo haziko salama kwa kuwa zimenyonya maji mengi na muda wowote zinaweza kuanguka na kuleta madhara makubwa.

Sambamba na agizo hilo Malima ameishukuru Serikali, wadau mbalimbali wa maendeleo na chama cha mapinduzi kwa kuungana pamoja katika kuwasaidia wananchi wa Kilosa waliokumbwa na kadhia hiyo ya mafuriko.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka ameishukuru Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa, Kamati za ulinzi na usalama za Mkoa na Wilaya pamoja na wadau waliotoa misaada hiyo na kwamba Serikali inawajali wananchi wake.

Naye Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati Bi. Janeth shango kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa benki hiyo ametoa pole kwa wananchi waliyoathirika Wilayani Kilosa ambapo benki hiyo imetoa shilingi milioni 10.

Misaada iliyotolewa kwa waathirika wa mafuriko Wilayani Kilosa ni pamoja na vifaa vya ndani kama sufuria, ndoo, masinia mashuka, sahani na bakuli. Vingine ni vyakula kama mchele, unga wa sembe, mafuta ya kupikia, maharagwe na sukari

Chanzo: www.tanzaniaweb.live