Mwanza. Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo amewataka waandishi wa habari nchini kujiunga na mifuko ya hifadhi za jamii kujiandalia mazingira bora ya maisha ya uzeeni.
Akifungua mkutano wa pili wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na marafiki jijini Mwanza leo Jumatano Julai 31, 2019, Nsokolo amesema wengi wa waandishi wa habari nchini hawajajiunga na mifuko ya jamii kutokana na sababu kadhaa ikiwemo kukosa mikataba ya ajira.
"Waandishi wa habari ni hodari kuripoti taarifa za watu kukosa mafao. Lakini wengi wetu hatujajiunga kwenye mifuko hiyo. Tubadilike sasa tukikumbuka usemi wa fainali uzeeni," amesema Nsokolo
Ametoa mifano ya baadhi ya Waandishi nguli wa habari waliostaafu ambao maisha yao ya sasa hayaakisi uhodari na mchango wao kwa jamii wakati wa utumishi wao kutokana na kukosa mafao.
Awali, Mwenyekiti wa Mwanza Press Club (MPC), Edwin Soko amewataka wanachama wa klabu hiyo kujiunga kwenye mifuko ya jamii kujiandalia mafao wakati wa uzeeni.
"MPC tutashirikiana na NSSF siyo tu kuhamasisha watu kujiunga, bali pia wanachama wetu kujiunga na kunufaika na mafao mbalimbali ikiwemo ya elimu na uzazi," amesema Soko
Pia Soma
- Mwili wa kaka yake Mbowe wawasili nyumbani
- Olenasha azishukia halmashauri 100 zilizopewa fedha za ujenzi wa ofisi
- VIDEO: Maswali kibao mwandishi wa habari anayeshikiliwa polisi
"Mfumo mpya wa mifuko ya jamii inaruhusu kila mtu kujiunga na kunufaika na mafao bila kujali kama ni mwajiriwa. Hata wajasiriamali wakiwemo mama lishe, waendesha bodaboda na wamachinga wanaweza kujiunga kupitia mfumo maalum," amesema Kahensa
Ametaja baadhi ya mafao ya muda mfupi inayotolewa na mfuko huo kuwa ni uzazi, msaada wa mazishi, matibabu na kukosa ajira kwa walioachishwa kazi.
Mkutano huo unahudhuriwa na waandishi wa habari zaidi ya 50.