Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waandishi wa habari Ruvuma wamkumbuka JPM

Fec94a40a3ae2fc929b220c39307693b Waandishi wa habari Ruvuma wampa 5

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Ruvuma kimesema hakitamsahau Rais John Magufuli kwa mambo makubwa aliyofanya kwa tasnia ya habari na maendeleo katika mkoa huo.

Katibu wa chama hicho Andrew Chatwanga amesema, Rais Magufuli alikuwa rafiki wa wanahabari na alitoa mchango mkubwa katika sekta ya habari hapa nchini.

Kwa mujibu wa Chatwanga, Rais Magufuli amefanya mageuzi makubwa katika tasnia hiyo ikiwemo kutungwa kwa baadhi ya sheria ambazo zinatakiwa kuanza kufanya kazi mapema mwaka ujao.

Alisema hivi sasa waandishi wengi wanafanya kazi kwa weledi na kufuata sheria, jambo lililosaidia hata kufichua maovu yanayofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali .

Aidha alisema Rais Magufuli alihakikisha kunakuwa na mahusiano mazuri kati ya waandishi wa habari na serikali ambapo ni jambo la kujivunia kuona hivi sasa kesi kati waandishi wa habari na wadau zimepungua.

Amewataka waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kufuata maadili ya kazi yao na kutanguliza mbele maslahi ya nchi kama hatua ya kumuenzi Rais Magufuli ambaye alihimiza sana waandishi kuweka mbele uzalendo kwa nchi yao.

Kwa upande wake Mweka hazina wa chama hicho, Cresensia Kapinga alisema Rais Magufuli alikuwa kiongozi imara aliyeamini kwenye kufanya kazi ili kusimamia ukuaji uchumi wa nchi na alikuwa kiongozi asiyependa kuingiliwa katika utawala wake na mataifa mengine.

Alisema mbali na kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya habari pia, daima atakumbukwa na wana Ruvuma kwani katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake ametekeleza miradi mikubwa katika mkoa wa Ruvuma.

Alisema alitoa zaidi ya Sh bilioni 37 kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Songea, ujenzi wa barabara ya lami Mbinga hadi Mbambabay ya km 67.

Chanzo: www.habarileo.co.tz