Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waandishi Mbeya wavutiwa utendaji wa JPM

3c911bb9b9079cd8337a3f2e29b6e6e3 Waandishi Mbeya wavutiwa utendaji wa JPM

Mon, 9 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAANDISHI wa habari mkoani Mbeya wamesema wana imani kubwa na utendaji kazi wa kipindi cha pili cha serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kwa kuwa sasa watendaji wengi wanatambua nini kiongozi huyo anahitaji kwenye utumishi wa umma kwa Watanzania.

Wamesema tumbuatumbua ya mawaziri na watendaji wengine katika kipindi kilichopita hususani miaka ya mwanzoni mwa utawala wa awamu ya kwanza ya Rais Magufuli ilitokana na wateule wengi kutotambua dhimira ya kiongozi huyo katika kuwatumikia Watanzania, kujituma na uwajibikaji.

Mmoja wa wanahabari hao, Hines Thobias alisema matarajio ya Watanzania ni kuona mawaziri na wateule wengine watakaoteuliwa wanakwenda na kasi anayoitaka Rais Magufuli katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Baada ya wananchi kutambua uchapakazi wa Magufuli ni wazi wataongeza kasi ya kujituma katika kazi hatua itakayochochea zaidi kukua kwa uchumi wa Tanzania,” alisema.

Samuel Ndoni alisema matarajio ya wana Mbeya ni kuona mkoa huo unakuwa lango kuu la kiuchumi katika nchi za Kusini mwa Afrika kwa kuwekewa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwamo miundombinu ya barabara, reli, bandari katika Ziwa Nyasa, uwanja wa ndege wa Songwe na bandari kavu inayotarajiwa kujengwa Inyara Mbeya vijijini.

"Kwa kuwa mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi chakula nchini kupitia kilimo tunatarajia kujengwa viwanda vya msingi kwenye maeneo yanayozalisha mazao ili kuyaongezea thamani na kuleta tija kwa wakulima wakubwa na wadogo," alisema.

Naye Hosea Cheyo alisema matarajio ya Tanzania kupaa zaidi kimaendeleo ni makubwa kwani dalili njema zilianza kuonekana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Alisema ili kuwezesha hilo ni muhimu mtandao wa usafiri na usafirishaji hususani wa barabara kuunganisha mkoa huo na maeneo mengine kuendelea kupewa mkazo.

Joseph Mwaisango alisema Watanzania wengi wana matumaini makubwa na serikali kuendelea kuboresha sekta ya elimu ya msingi sambamba na miundombinu ya usafiri hususani barabara kutokana na umuhimu wake katika kusafirisha mazao ya wakulima kutoka mashambani hadi yaliko masoko.

Felister Richard alisema waandishi wa habari nchini wana matarajio makubwa kwa awamu ya pili ya Rais Magufuli itaangalia maslahi na mazingira wanayofanyia kazi.

"Tunapenda tuone waandishi wa habari wanalipwa mishahara na waajiri kulingana na elimu zao kwa kuzingatia kima cha chini cha mshahara, maslahi kwa wanajitolea na pia kuwalipa wafanyakazi muda wa ziada na kuwalipia mifuko ya hifadhi za jamii. Lakini pia tungependa kuona wanahabari wanaoitumikia tasnia hii maisha yao baada ya kazi hiyo yanaandaliwaje kwani mchango wao ni mkubwa katika maendeleo ya taifa lao," alisema Felister.

Chanzo: habarileo.co.tz