Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waandaaji Nanenane Magharibi washauriwa

Ec62cabc6bffd6a6d5a5fbaf43602653 Waandaaji Nanenane Magharibi washauriwa

Mon, 10 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAANDAAJI wa Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) Kanda ya Magharibi, wametakiwa kualika kampuni na taasisi za nje ya kanda hiyo zinazojihusisha na tekonolojia ya zana za kisasa za kilimo, usindikaji wa mazao, ufugaji na uvuvi, ili kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kwa wahusika wa sekta hizo kwa gharama nafuu.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, wakati akifunga maonesho hayo kwa Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Tabora na Kigoma chini ya kauli mbiu inayosema;

‘Kwa maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi, chagua viongozi bora 2020.’ Alisema hatua hiyo itasaidia kuendelea kuboreshwa kwa tekonolojia za kilimo, uvuvi na ufugaji na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi na ajira.

Adengenye alisema Kanda ya Magharibi ina fursa nyingi, ikiwamo maeneo makubwa ya uzalishaji wa mazao, mifugo mingi na maeneo ya uvuvi ambayo yakiboreshwa yataongeza mnyororo wa thamani na kuwezesha kupata malighafi bora na za kutosha kwa ajili ya viwanda vya hapa nchini na nje ya nchi.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa aliwahimiza wananchi kuongeza juhudi katika ufugaji wa samaki kwa ajili ya kujipatia chakula chenye protini na kujiajiri ili kujipatia kipato.

Aliwataka wafugaji hao kutumia kituo cha serikali cha ukuzaji viumbemaji kilichopo wilayani Igunga kupata elimu ya ufugaji bora na kununua vifaraga bora vya samaki wa aina mbalimbali kwa ajili ya kufuga.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati, aliwataka wakazi wa Kanda ya Magharibi kutumia uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu kuchagua viongozi ambao watakuwa na moyo wa kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kupiga hatua na kushiriki katika uchumi wa kati kikamilifu.

“Ni vema mkachagua kiongozi ambaye atakuwa tayari kuwasaidia katika kuwawekea mazingira mazuri ya uzalishaji ili muweze kuongeza vipato vyenu,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz