Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waagizwa kukamilisha vyuo vya VETA vya Kagera, Geita

5f5657685d3c3d389a367724339aa86b Waagizwa kukamilisha vyuo vya VETA vya Kagera, Geita

Sat, 5 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BODI ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi imeagiza ukamilishaji haraka wa ujenzi wa vyuo vya VETA mkoani Kagera na Geita ili wananchi wanufaike na mafunzo katika vyuo hivyo.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Peter Maduki alitoa agizo hilo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi katika mikoa hiyo.

"Kama Bodi, tunatoa masikitiko yetu makubwa kwa namna ambavyo mradi umetekelezwa na kukwama kwake kwa takribani mwaka mmoja na nusu tangu ulipoanza kutekelezwa. Tunasikitika kwa sababu kubwa moja, wananchi hawawezi kupata fursa tuliyokuwa tunatarajia. Tulitarajia tungeanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi 400 wa kozi za muda mrefu na 1,000 wa kozi za muda mfupi,” alisema Maduki.

Aliongeza kuwa, "Tumetafakari jambo tukishirikiana na Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuona namna gani tunaweza kufufua mradi huu.”

Alisema baada ya majadiliano wameona mradi huo uendelee kwa fedha kutoka chanzo kingine ambacho serikali imekitafuta ili ukamilike kwa haraka zaidi.

Alisema hali ya uhitaji wa mafunzo kwa wananchi wa mikoa ya Kagera na Geita imedhihirishwa na kiwango cha maombi ya kujiunga na chuo cha VETA Chato ambapo zaidi ya vijana 300 wamewasilisha maombi ya kusoma kozi za muda mrefu zitakazoanza Januari, mwaka 2021.

Akitoa taarifa kwa bodi kuhusu ujenzi wa vyuo hivyo kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk Pancras Bujulu alisema kuwa mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Kagera umekamilika kwa asilimia 45 na unatarajiwa kukamilika Agosti, mwaka 2021.

Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera kinajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa Sh bilioni 19.4 katika eneo la ukubwa wa hekta 40.5 katika kijiji cha Burugo wilayani Bukoba.

Alisema chuo kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 2,000 wa kozi fupi katika fani mbalimbali ikiwemo useremala, uchomeleaji, upakaji rangi na ufundi bomba.

Mjumbe wa Bodi ya VETA ambaye ni Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Paul Koyi alifurahia kuona VETA ikitoa stadi zinazolenga kuandaa wahitimu watakaoweza kuanzisha shughuli zao za kuwaingizia kipato pindi wanapohitimu.

Chanzo: habarileo.co.tz