KUTOKANA na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuibua madudu kila mwaka, wasomi wameshauri serikali hatua ambazo serikali inapaswa kuchukua ikiwamo kutoa adhabu kali ili kukomesha kujirudia kwa ubadhirifu wa fedha za umma na kutofuatwa kwa sheria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi wameshauri serikali kuangalia mifumo yake ya ukusanyaji wa mapato pamoja na inayoruhusu matumizi ya fedha za serikali kuepuka kufanyika matumizi ya hovyo na upotevu wa fedha kama ilivyooneshwa katika CAG.
Aidha, wamewataka Watanzania kuweka itikadi pembeni katika kujadili hiyo taarifa na hatimaye kuja na majawabu ni namna gani madudu yaliyobainika yanaweza kudhibitiwa.
Adhabu ziume Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi alisema licha ya Serikali ya Awamu ya Tano kufanya kazi nzuri, lakini wabadhirifu wameendelea kuwepo hivyo dawa pekee ni kutolewa adhabu kali kwa wanaosababisha madudu hayo kwenye taasisi zao.
“Adhabu ziwe kali na ziume, kwa mfano mtu anafanya ubadhirifu halafu akipewa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja tu, adhabu hii ni ndogo kwa sababu baada ya muda mfupi mtu huyo atatoka na kwenda kufurahia maisha, lakini mtu akifungwa miaka kumi, watu wataogopa,” alisema Profesa Moshi.
Pia alisema kutokuwepo kwa mkakati madhubuti katika taasisi wa kufuatilia matumizi ya fedha za umma kwa kila robo mwaka, huchangia kuwepo kwa matumizi mabayo ya fedha, lakini pia wakaguzi wa ndani ya taasisi husika wanawajibu wa kuhakikisha madudu hayo hayatokei kwa kufanya ukaguzi wa kila mara.
Wakili wa Kujitegemea, Reuben Simwanza alisema kujirudia kwa madudu yanayoibuliwa na CAG kila mwaka ni kutokana na kutokuwepo kwa dhana ya uwajibikaji ambalo ndiyo tatizo kubwa kwenye taasisi nyingi.
“Ripoti ya CAG inagusa maeneo mengi ikiwemo miradi yote, halmashauri zote, wizara na maeneo mengine mengi, kukosa madodo siyo rahisi, lakini kikubwa hapa kinachochangia kuwepo kwa madudu haya ni kutowajibika kwa wasimamizi wa sheria katika maeneo husika,” alisema Simwanza.
Simwanza alisema ni wakati muafaka sasa kwa sheria kuchukua mkondo wake watu wengine waogope kufanya madudu kama ambavyo yameibuliwa kwenye Ripoti ya CAG.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Shule Kuu ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Wilhelm Ngasamiaku pia alisema kutochukuliwa hatua kwa wahusika ni chanzo cha kujirudia kwa madudu katika ripoti za kila mwaka. Dk
Alisisitiza uwajibikaji na umuhimu wa kufanyia kazi ipasavyo mapendekezo yanayotolewa na CAG.
Mifumo iangaliwe Wakili wa Kujitegemea, Albert Msando alishauri serikali kuangalia mifumo yake ya ukusanyaji wa mapato pamoja na inayoruhusu matumizi ya fedha za serikali kuepuka kufanyika matumizi ya hovyo na upotevu wa fedha kama ilivyooneshwa katika CAG.
Alisema ripoti ya CAG ni kioo kinachoonesha mahali nchi ilikotoka na inakoelekea katika suala la matumizi ya fedha za umma hivyo Watanzania wanatakiwa kuweka itikadi pembeni katika kuijadili.
Alisema swali kubwa ambalo serikali inatakiwa kujiuliza ni kwa nini ipo mifumo imara inayoaminiwa na serikali lakini inaruhusu makosa yanayoigharimu nchi kwa kiasi kikubwa?
“Swali hilo ikiwa litazingatiwa litasaidia kuzuia mapungufu katika taasisi za umma yasiendelee kutokea na kuigharimu nchi,” alisema Msando na kusisitiza umma kujadili taarifa ya CAG bila jazba na mihemko ya kisiasa kwa sababu watashindwa kujua ukweli kuhusu yaliyomo.
Alisema taarifa ya CAG ni ushahidi kuwa yapo makosa yalikiukwa katika manunuzi na matumizi mbalimbali ya fedha za serikali. Hata hivyo, alisema haiwezekani kuitumia taarifa hiyo kuhukumu watu au taasisi kwa sababu vipo vyombo vingine vinahusika katika kuchunguza endapo zipo jinai zilizofanywa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye alisema ripoti hiyo inatakiwa kuwa onyo kwa viongozi mbalimbali na kuwakumbusha wajibu wao wa kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa katika kutumikia nchi.
“Ni muhimu kwa taasisi za umma kuwekeza katika utoaji wa elimu na mafunzo kwa wafanyakazi hususani katika kada zao kila wakati kama njia mojawapo ya kuepuka makosa kwa kufuata sheria na taratibu za kiofisi,” alisema Profesa Anangisye.