Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyoo vya kisasa vyageuka lulu Dar, utiririshaji chemba sasa kukoma

A19510ddb3a92399c0ad2754792df6f6 Vyoo vya kisasa vyageuka lulu Dar, utiririshaji chemba sasa kukoma

Thu, 11 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

“Ni kuchafu sana huku mvua ikinyesha watu wanaachilia chemba zao za vyoo, hivyo vinyesi vinasambaa mtaani na harufu kali tunakaa kwa shida,”anasema Zumaiya Omary, mkazi wa Vingunguti kwa Kombo jijini Dar es Salaam.

Eneo hilo lina nyumba nyingi ambazo zimebanana, hali inayosababisha kusiwepo na barabara ambayo gari linaweza kupenya kwa ajili ya uzoaji taka.

Hivyo pale choo kinapojaa mwenye nyumba hulazimika kuchimba shimo lingine.

Hata hivyo ardhi ni finyu na maeneo ni madogo, wakati mwingine hulazimika kuvunja chumba kimoja na kuwa choo au kumuita mzoaji wa taka za chooni kutoa.

Lakini hivyo vyote ni gharama kubwa kutokana na wakazi wengi kuwa na kipato cha kawaida, hivyo wengine husubiri mvua za masika zinapoanza kunyesha.

Zumaiya anasema Kupakua uchafu vyooni unaweza kugharimu Sh 20,000 hadi Sh 30,000 kulingana na makubaliano na mpakuaji.

“Na ilikuwa haichelewi kujaa kwa sababu haya makaro ya kuogea yalikuwa nje, sasa hayakidhi watu wako wengi zinajaa baada ya muda mfupi, likijaa inabidi maji yatafute njia, hivyo mazingira yanakuwa machafu ,”anaeleza Zumaiya.

HALI YABADILIKA

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Jiji la Dar es Salaam limetajwa kuwa la sita kwa usafi Afrika kulingana na utafiti uliotolewa na Afrika Tours.

Utafiti huo ulibainisha majiji 12 safi Afrika, ambapo jiji la kwanza ni Kigali, Rwanda.

Majiji mengine ni Port Louis –Mauritius, Cape Town, Afrika Kusini,Tunis-Tunisia, Windhoek-Namimbia, Libreville-Gabon,Dar es Salaam-Tanzania, Gaborone-Botswana, Algiers-Algeria, Nairobi-Kenya, Kumasi-Ghana na Asmara-Eritrea.

Hatua hiyo ya usafi wa jiji inatokana na mikakati mbalimbali hasa vyoo.

Baada ya wananchi kupata kero nyingi kuhusu uchafu wa vyooni, serikali kupitia mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam(DAWASA), kwa kushirikiana na wadau wameanzisha mfumo rahisi wa uondoshaji maji taka majumbani.

UJENZI WA VYOO

Mhandisi Msaidizi katika Miradi ya Usafi wa Mazingira kutoka Idara ya Usafi wa Mazingira nje Mtando, Shaabani Saidi anasema hadi sasa jumla ya vyoo vya kisasa 310 vimejengwa na kuunganishwa na mfumo wa kutiririsha uchafu moja kwa moja hadi bwawani.

“Miradi hii ilianza 2016, kwa kipindi hicho kulikuwa na mitaa miwili ya Mji Mpya na Kombo na huu Mtaa wa Kombo ni mkubwa ,kwa kipande cha Mji Mpya tulishafikia sehemu kubwa.

Anasema mradi huo unaosimamiwa na DAWASA unachukua zaidi ya kilometa sita pamoja na maunganisho ya vyoo kwa awamu mbili.

Anabainisha kuwa wanatarajia kufanya awamu ya tatu kwa kujenga vyoo vya kisasa 250, kwa udhamini wa Benki ya Dunia katika Mtaa wa Kombo na maandalizi yameanza.

“Bado kuna wateja wanahitaji kufikiwa,”anasisitiza Shaban.

Anasema lengo la mradi huo ni kudhibiti magonjwa ya milipuko itokanayo na uchafu pamoja na mafuriko.

“Mafuriko yakitokea vyoo vya shimo vinajaa na nyumba zimebanana na ardhi sio nzuri, ina udongo wa mfinyazi, akichimba choo baada ya mwezi kimejaa,” anasema.

Anasema mradi huo unafanya maji kwenda moja kwa moja kwenye mfumo kuelekea katika mabwawa

“Mteja anatakiwa kutengeneza choo kwa gharama zake, kwanza anatufuata tunaenda na fundi anafanya tathmini, jukumu lake ni kurekebisha na sisi tunamuunganisha, kwa mwezi mteja atalipa Sh 5,900 kutokana na makadirio ya EWURA,”anafafanua Shaabani.

Anaeleza kuwa maji taka yanapokusanywa kwenye bwawa, huwa yanatibiwa na kutumika katika umwagiliaji au kuingia baharini.

Anasema mradi pia umehusisha Buguruni Kisiwani, kutokana na urahisi wa uwepo wa bwawa hali inayorahisisha mfumo.

“Jografia ya huku nyumba ziko juu na bwawa liko chini, hivyo ni rahisi,” anasema.

Shabani anasema kwa upande wa Buguruni tayari nyumba 87 zimeshaunganishwa na mfumo huo na uhitaji ni mkubwa.

HALI SHWARI VINGUNGUTI

Zumaiya anasema baada ya kuunganishwa na mfumo rahisi wa uondoshaji maji taka majumbani, mazingira sasa yamekuwa masafi

“Maji machafu hayatiririki kwa sababu sasa hivi tukifua maji tunachuja na kumwaga chooni na maji yote tunamwaga chooni tunafurahia mradi huu,” anaeleza na kuongeza:

“Sasa hamna kufumua vyoo wakati mvua zinaponyesha, awali watu walikuwa wanafanya kwa sababu utakuta mwingine hana gharama za kumlipa mtu wa kuchimba shimo au kupakua na yeye kupakua inakuwa ngumu, kwa hiyo anavizia kipindi mvua inanyesha anafungua uchafu unatiririka,” anasema.

Anasema mfumo huo unagharama rahisi, ambapo kwa mwezi wanalipa Sh 15,000 ambazo wanazimudu.

Mkazi mwingine Asia Ramadhani anayetumia vyoo vya kisasa anasema sasa wana uhakika wa sehemu salama na safi ya kujisaidia na kumwaga maji.

“Toka tuwekewe hivi vyoo mazingira yamekuwa masafi, yale ya mwanzo mara yabomoke hivyo sasa uhakika upo kama likijaa labda nyie watumiaji mmejitumia vibaya

“Sasa ukiona mtaa mchafu tatizo ni watumiaji, hivi havihitaji kuweka pempasi, pedi, vitambaa na taka ngumu, kwani vinaziba na kuleta uchafu,”anasisitiza.

Fatuma Kondo anasema awali vyoo vya shimo walikuwa wakisumbuliwa na manispaa kwa kutozwa faini, lakini sasa hali imekuwa shwari.

“Tunakamatwa tunalipa faini Sh 50,000, 30,000 na wakati mwingine Sh 20,000 kwa ajili ya chemba, utakuta mwingine anatumia shimo ila chemba ya kutolea maji machafu hana maji yanakuja sehemu wanakaa watu,”anaeleza.

Anasema kutokana na adha vyoo hivyo vya kisasa vimekuwa msaada kwao, kwani havijai.

“Kwa wengine ambao hawajapata wanatuuliza maswali, tunawaambia ni vizuri ilimradi usafi wako, kwa sababu ukiwa mchafu utasema ni vibaya,”anafafanua.

MATUMIZI SAHIHI CHANGAMOTO

Wakizungumza na HabariLEO, baadhi ya wakazi hao wanasema matumizi sahihi ya vyoo hivyo yamekuwa hayazingatiwi kwa baadhi ya watumiaji.

Fatuma anasema wapo wanaotupa taka ngumu hali inayosababisha mfumo kuziba.

“Unaona zile chemba pale(anamuonesha mwandishi) ikifumuka uchafu unakuja hadi uwanja wa nyumba, usipomwita mtu kukutengenezea watoto wanakuwa wanachezea kinyesi siku nzima.

“Tatizo linalojitokeza hapa ni ustaarabu wa matumizi, watu wengine wanatumia vibaya kwa kutupa tambara, gunzi na taka zingine sasa ikiziba mfumo mzima kutoka huko juu unaathirika chemba zinajaa ni juzi hapa nimefungua hiyo chemba lilikuwa limejaa mpaka juu yanatoka, nikaomba mpira nikaanza kuchokonoa nikapata kitambaa, pempasi na taka zingine.

“Wenzetu wa juu(nyumba yake iko bondeni) wanatusumbua sisi katika matumzi, kama hawatupi hatupati shida na chemba hazizibi, lakin wakishatupa ni tatizo.”

Anasema ni vyema pia hata watoto wakaelekezwa matumizi ya vyoo hivyo.

UHITAJI WA MRADI

Mwenyekiti wa Mtandao huo kutoka ofisi ya DAWASA, Josephina Livistone, anasema uhitaji wa mfumo huo bado ni mkubwa kutokana na ubora wake

“Lakini wapo wachache wanajiuliza maswali, ila wengi wanakubali, tumeshukuru umeleta maboresho mazuri nyumba sasa hakuna mambo ya kufubua vyoo mvua zikinyesha kesi serikali za mtaa za uchafu zimepungua ,”anaeleza

Naye Furaha Jongo, Mjumbe wa serikali ya Mtaa wa Kombo anasema wamefikiwa na mradi huo kwa kiasi kikubwa.

“Watu wengi wanahitaji zaidi mradi, walisubiri mwezi wa tatu na watano wapo wanaojaza fomu wenyewe na wanakwenda DAWASA, ili wawatengenezee mfumo.

HATUA ZA KUTATUA CHANGAMOTO

Jongo anasema serikali za mtaa wanatoa elimu ya matumizi ya choo kama kuwaelekeza wasitupe vitambaa, pampasi, pedi na taka zingine, ili kusitokee chemba kuziba na kusababisha uchafu.

“Kama vikiziba Tunawaambia wachange Sh 20,000, ili mtu aje kuzibua pawe na usalama, ile inakuwa kero wanakuja kushtaki kuwa walioweka mfumo kwa nini wasitafute mtu azibue,” anasema Jongo.

Kwa upande wake Shabani anasema wanawatumia maofisa maendeleo na ofisa afya wa kata kutoa elimu matumzi sahihi ya mifumo, kwani ikitumika vibaya inaweza kuleta tabu kwa watu.

“Kwa mfano unakuta mtu alipojengewa tunaweka kifaa kinachoitwa ‘wire measure’, inazuia kabla ya kuingia kwenye mtandao, akitupa taka ngumu inaziba kwake, kuna watu sio wastaarbu wanatoa waya, hivyo wanawapa wengine tabu,” anasema.

Anasema wazibuaji wakifika wanakuta taka ngumu, kitu ambacho sio sahihi, kwani wao wanatarajia kukuta michanga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live