Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vya ushirika vyapewa somo

41148 Pic+ushirika Vyama vya ushirika vyapewa somo

Tue, 12 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vyama vya ushirika Tanzania vimetakiwa kuhakikisha viongozi wanaowapa dhamana kuwaongoza wanazingatia utawala bora ili kufanikisha malengo waliyojiwekea.

Wito huo umetolewa leo Jumapili Februari 10, 2019 na Kaimu Mrajisi wa vyama vya ushirika Tanzania, Tito Haule wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge (MHCS Ltd) cha jijini Dar es Salaam.

Amesema ili ushirika uweze kufanikiwa na kufikia malengo ni lazima wanachama wenyewe kwa wenyewe waheshimiane na kutimiza wajibu wao waliojiwekea ikiwamo kuwachagua viongozi watakaozingatia utawala bora.

“Kukiwa na utawala bora hata matumizi ya fedha yatakuwepo, kukiwa na utawala bora hata nidhamu kwenye ushirika itakuwapo lakini vyama vya ushirika vinapaswa kukaguliwa na mkaguzi wa nje,” amesema Haule.

Mrajisi huyo amesema viongozi wanapaswa kuwa makini katika mikataba ambayo wanaingia ili wasije kuugharimu ushirika na kuepuka migogoro ambayo inaweza kuwarudisha nyuma katika malengo yao.

Naye Meneja wa MHCS, Thomas Mosha amesema ushirika huo ulioanzishwa mwaka 1971 ukiwa na wanachama 10 ambapo kwa sasa una wanachama 387 kutoka mikoa mbalimbali.

“Tumekuwa tunawajengea nyumba wanachama wetu katika maeneo mbalimbali kupitia mikopo ambayo wanailipa kwa kipindi cha miaka 15,” amesema Mosha.  

Mosha amewaomba wana ushirika huo kudumisha umoja na mshikamano ili yale wanayoyapanga waweze kuyafikia bila vikwazo vyovyote kwani kukiwa na migogoro hawawezi kufika mbali.

Kwa upande wake, mmoja wa wanachama wa ushirika huo, Rukia Magoma amesema mafanikio ambayo ameyapata tangu kujiunga mwaka 1971 ni kumiliki nyumba.

“Niwashauri vijana wa sasa, wajiunge katika ushirika, kwani kama ambavyo mimi namiliki nyumba na wao wanaweza kujikuta huko mbele wanamiliki vitu vikubwa vya thamani,” amesema Magoma.



Chanzo: mwananchi.co.tz