Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vurugu zatokea Namanga baada ya mfanyabiashara kudaiwa kutekwa

49014 Mfanyabiasharapic

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Namanga. Wakazi wa mpaka wa Kenya  na Tanzania wa Namanga upande wa Kenya wamezuia magari ya nchini Tanzania kuingia nchini kwao, kwa kudai kutekwa kwa mfanyabiashara wa kubadili fedha za kigeni wa nchini mwao hapo jana Jumanne, Machi 26 majira ya saa 3 usiku.

Mfanyabiashara huyo maarufu katika mpaka wa  Namanga anajulikana kwa jina la Moha ambaye anadaiwa alichukuliwa na gari lenye namba za Tanzania.

Akizungumza mmoja wa wananchi hao Odinga Nguduu amesema kuwa saa tatu usiku ilifika gari yenye namba za Tanzania kwenye ofisi ya mfanyabiashara huyo na waliondoka naye kuelekea Namanga ya Tanzania

"Tangu achukuliwe jana usiku hajarudishwa na hadi sasa haonekani mtu wetu," amesema.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe aliwataka wakazi wa mji huo kutulia ili Serikali ya Tanzania ichunguze waliohusika.

"Hakuna haja ya kufanya vurugu na kwani tunachunguza tukio hili kujua ni watu gani wamehusika naomba watuamini," amesema

Amesema wananchi wachache hawezi kuzuia shughuli za mpakani kwa kuzuia magari ya Tanzania kuingia Kenya.

"Kuzuia magari kwa kuchoma matairi ni kuvunja sheria na tumelazimika kutumia vyombo vya dola kudhibiti vurugu," amesema.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wakazi wa mpaka huo kuheshimu sheria na taratibu ili kutoingia katika migogoro na vyombo vya dola.

Mwaisumbe amesema hadi leo Jumatano, Machi 27 mchana hakuna mtu ambaye alijeruhiwa kutokana na vurugu hizo.

Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Jonathan Shana ameondoka jijini Arusha kwenda Namanga kufatilia mgogoro huo.

"Kamanda atakwenda Namanga kujua ukweli na atatoa taarifa kilichotokea," amesema ofisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mkazi wa Namanga, Simon Ledupa amesema kuwa Namanga ni mpaka mkubwa na kuna watu wengi kutoka mataifa mbalimbali wanapita hapo hivyo huyo mtu wanayedai ametekwa na Watanzania inawezekana yupo ndani ya Kenya.

Ledupa amesema wanapotuhumu gari yenye namba ya Tanzania wanakosea kwa kuwa mpakani biashara za magendo ni nyingi na watu kutumia namba za nchi kwa nchi kwa biashara haramu ipo sana.



Chanzo: mwananchi.co.tz