Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vurugu zatawala uchaguzi jijini Arusha

11606 Pic+vurugu TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Matukio ya mgombea kujeruhiwa, mbunge kupigwa, viongozi wa vyama na wafuasi kujeruhiwa ni baadhi ya mambo yaliyotawala jijini Arusha katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana.

Wakati vurugu zikitoa katika kata nne za jiji hilo, maeneo mengine kulikofanyika uchaguzi mdogo, ukiwamo wa mbunge katika Jimbo la Buyungu, Kigoma na katika kata nyingine kadhaa nchini, ulikuwa shwari na matokeo ya awali yaliyopatikana hadi saa 2:00 usiku jana yaliyonyesha kwamba CCM ilikuwa inaongoza katika kata nyingi.

Katika vurugu hizo za Arusha, mmoja wa mgombea, viongozi wa vyama na wafuasi wao walipigwa, kujeruhiwa na mmoja kuchomwa kisu.

Mgombea ajeruhiwa, alazwa

Katika tukio hilo, mgombea udiwani wa Kata ya Kaloleni kupitia Chadema, Boniface Kimario alijeruhiwa huku wakala mkuu wa Chadema katika kata hiyo, Ibrahim Issa akichomwa kisu na hadi jana jioni, wawili hao walikuwa wamelazwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Pia, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema amepigwa huku Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Kaloleni, Idd Mkuluu akijeruhiwa katika vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’azi, “Hili tukio la vurugu za Arusha tumelipata, tumefungua jalada la uchunguzi kujua ambao wamehusika na hatua zitachukuliwa.”

Alisema maeneo mengi yaliyofanya uchaguzi jana yalikuwa shwari isipokuwa katika jiji la Arusha.

Kamanda Ng’azi alisema mapema jana, Lema alitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio la kuvamiwa mgombea wa udiwani.

Lema alisema asubuhi alipigiwa simu kuwa mgombea chama hicho katika Kata ya Kaloleni amevamiwa na alikuwa katika hali mbaya.

Alisema alimpigia simu Kamanda Ng’azi ambaye alimweleza kuwa tayari ana taarifa na amepeleka gari eneo la tukio.

“Baada ya kufika nilimkuta mgombea na msaidizi wake katika hali mbaya. Nikiwa na polisi na kulikuwa na kundi la walinzi wa CCM, Green Guard na tulianza kuwauliza kwa nini wamefanya uhalifu huo,” alidai Lema.

Alisema wakiwa wanahojiana, kijana mmoja alimtemea (Lema) mate na alivamiwa na kuanza kupigwa hadi akaanguka chini.

Huku akionyesha jeraha kwenye kidole, Lema alidai kuwa polisi hawakuwadhibiti vijana hao.

Lema ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema kutokana na vurugu na hali ilivyokuwa, watashauriana na chama hicho kuona ni namna ya kufanya.

Hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Elias Mpanda alisema chanzo cha vurugu hizo ni Lema ambaye aliruka kuwapiga kichwa vijana wa CCM.

“Badala ya mbunge kufanya kazi ya kutatua kero, amekuwa chanzo cha vurugu,” alidai.

Wilayani Arumeru, Katibu wa Chadema wilayani humo, Innocent Kisanyaga alisema licha ya vurugu na kupigwa kwa wagombea, pia taratibu nyingi za uchaguzi zilikiukwa.

“Mawakala wetu wamezuiwa, viongozi wa CCM wanaingia vituoni bila utaratibu, polisi inashirikiana na vijana wa CCM maarufu kama Green Guard kufanya uhalifu,” alisema.

Wagombea wa Chadema katika Kata ya Daraja mbili na Osunyai, nao walidai kuwapo matukio ya vurugu likiwamo tukio la gari la mgombea kutekwa kwa muda.

“Nilikuwa nakagua vituo, baada ya kushuka kituo cha Daraja Mbili, vijana wa CCM walipanda kwenye gari nililokuwa natumia aina ya Carina na kuvunja vioo, kisha kukaa juu ya gari na kunywa pombe,” alidai.

Katika kata ya Osunyai, Joseph Mbore, mgombea wa Chadema alikanusha taarifa iliyokuwa inasambaa kuwa amejitoa katika uchaguzi huo.

“Wamefanya mchezo mchafu kutoa taarifa za uongo mitaani kuwa nimejitoa, kitu ambacho si ukweli,” alisema

Mbali na vurugu hizo, pia kulikuwa na taarifa za kuzuiwa mawakala katika kata za Barai na Migungani.

Wasimamizi wazungumza

Licha ya vurugu hizo, msimamizi wa uchaguzi, katika Jimbo la Arusha, Grayson Orcado alisema katika uchaguzi wa jana hakukuwa na tukio ambalo lingeweza kuathiri uchaguzi.

Akizungumzia kupigwa kwa mgombea wa Kaloleni, alisema suala hilo linashughulikiwa na polisi na kuhusiana na mawakala alisema kulikuwa na taratibu za uchaguzi zilizopaswa kufuatwa.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Monduli, Steven Ulaya na msimamizi Jimbo la Longido, Jumaa Mhina, wote kwa nyakati tofauti walieleza uchaguzi kwenda vizuri na kuwa kama kulikuwa na upungufu ni kidogo ambao hauwezi kuathiri uchaguzi.

Jimbo la Buyungu

Katika Jimbo la Buyungu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno aliwataka wananchi baada ya kupiga kura kurejea majumbani ili kuepusha msongamano usio na sababu katika vituo.

Ottieno alisema kulikuwa na amani na utulivu katika maeneo mengi ya jimbo hilo. Upigaji kura katika vituo vingi ulianza saa 1.00 asubuhi na huku wananchi wakiwa wamejitokeza kwa kiwango cha chini, hasa katika maeneo ya mjini, tofauti na vijiji.

Msimamizi wa uchaguzi jimboni humo, Lusubilo Mwakabibi alisema mwitikio ulikuwa mkubwa na kuwa kati ya watu 61,000 waliojiandikisha takriban nusu walikuwa yamejitokeza hadi jana mchana.

“Hali ya vituo ni shwari na wananchi wengi wamejitokeza mwanzoni zilijitokeza changamoto za kucheleweshwa fomu za mawakala, ambazo zilifikishwa asubuhi katika vituo vya kupigia kura na mpaka sasa wananchi wengi wamekwishatimiza haki zao,” alisema Mwakabibi.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF), Mneke Jafar alisema baadhi ya mawakala wa chama hicho walizuiliwa kutekeleza majukumu yao katika Jimbo la Buyungu na kata 77.

“Mpaka muda huu (saa sita mchana) nimepata taarifa za kata mbili kwamba mawakala wetu walizuiliwa kufanya kazi yao,” alidai Jafar.

Mbali na Buyungu, wananchi katika Kata ya Mwanganyanga wilayani Kyela, walijitokeza kupiga kura kumchagua diwani na Msimamizi wa uchaguzi katika kata hiyo, Amos Basiri alisema hakukuwa na shida yoyote.

Katika Kata ya Mawenzi, Kilimanjaro makundi ya wafuasi wa vyama vilivyosimamisha wagombea walionekana wakitembea huku na kule kufuatilia yaliyokuwa yakijiri katika vituo vya kupigia kura.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Moshi Mjini, Michael Mwandezi alisema wananchi walijitokeza kwa wingi kupiga kura.

Katika Kata ya Turwa mkoani Mara, Mkazi wa Mtaa wa Buguti, Marwa Mniko alisema idadi watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa ndogo ikilinganishwa na uchaguzi wa 2015.

“Yaani hapa unapiga kura kisha unachapa mwendo maana hali ya Tarime ukizubaa unaweza kushtukia mabomu yanapigwa na wengine wameogopa kuja kupiga kura wakihofia mabomu lakini pia wengine wamepuuza kwa sababu ni uchaguzi mdogo,” alisema.

Imeandikwa na Mussa Juma, Filbert Rweyemamu, Happy Lazaro na Bertha Ismail (Arusha), Happiness Tesha Muhingo Mwemezi (Kakonko), Godfrey Kahango (Mbeya), Janeth Joseph (Moshi), Peter Elias (Dar) na Dinna Maningo (Mara).

Imeandikwa na Mussa Juma, Filbert Rweyemamu, Happy Lazaro na Bertha Ismail (Arusha), Happiness Tesha Muhingo Mwemezi (Kakonko), Godfrey Kahango (Mbeya), Janeth Joseph (Moshi), Peter Elias (Dar) na Dinna Maningo (Mara).

Chanzo: mwananchi.co.tz