Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vurugu tupu usafiri stendi ya Magufuli

MAGUFULI BUS STEND Vurugu tupu usafiri stendi ya Magufuli

Thu, 15 Dec 2022 Chanzo: ippmedia.com

Huu ni wakati wa watu hasa wa mikoa ya kaskazini kusafiri kwenda nyumbani kwa ajili ya kuungana na ndugu zao kutoka sehemu mbalimbali  kwa ajili ya kusherehekea Krismasi kama ilivyo desturi yao miaka nenda miaka rudi.

Wakati hayo yakiendelea, wako watu ambao wanachukulia usafiri huo kama fursa kwa ajili ya kupandisha nauli na wakati huo huo, wale wanaosafiri kwao ikiwa ni maumivu. Kwa wale wanaokatisha tiketi, baadhi yao kwao ni kipindi cha mavuno.

Kwa sasa, abiria hawezi kukata tiketi siku mbili kabla kwa kuwa wenye magari wanaona watashindwa kuamua nauli wanayopaswa kutoza huku ulanguzi wa tiketi unafanywa na wapiga debe ambao wanaona ni namna ya kujipatia kipato.

“Kaka nahitaji kusafiri siku ya Ijumaa kwenda Arusha nahitaji tiketi,” alisema dada mmoja aliyekuwa akitafuta nafasi katika moja ya mabasi kwa ajili ywa kusafiri.  

“Dada hatukatishi tiketi siku mbili kabla. Njoo  kesho au keshokutwa tutakukatia. Magari yetu yanajaa sana kwa sasa, tunahofia tusije tukakosa gari la kuwasafirisha,” alisema kijana aliyekuwa kwenye moja ya ofisi za mabasi katika kituo hicho.

Hali hiyo inaonyesha kuwa wenye magari wanapata abiria wa kutosha na hata nauli walizopanga kwa siku hiyo zinatozwa hivyo hivyo, tofauti na nyakati zingine wanalazimika kushusha hata bei elekezi kwa aina ya basi.

Ni maumivu kwa wasafiri kwa kuwa ulanguzi wa nauli unafanyika huku ukatishaji tiketi za kawaida ukiendelea kama kawaida licha ya serikali kuanzisha utaratibu wa tiketi mtandaoni.

Jana, Nipashe iliweka kambi katika kituo hicho na kushuhudia baadhi ya wasafiri  wakilazimika kusafiri kwa gharama mara mbili ya bei elekezi kwa sababu ya kukosa usafiri.

Aidha, mwandishi alikuta mamia ya abiria wakikata tiketi na wengine wakilipia nauli mlangoni kwenye mabasi hali iliyotoa mwanya kwa makondakta kuwalipisha bei kubwa.

Mmoja wa abiria aliyekuwa akienda Morogoro, Hellen Kigosi, alisema alilazimika kulipia nauli ya Sh. 15,000 kwa kuwa alilipia nauli mlangoni wakati abiria ni wengi na huku mabasi yakiwa machache.

“Ndio hivyo dada madereva wanaringa hasa kwa sababu mabasi makubwa yote yamejaza. Sasa haya ambayo siku zote watu hawayapandi sasa hivi ndiyo yamepandisha bei. Hawakuongeleshi  mara mbili, unataka lipa nauli hutaki mwenzio analipa anasafiri,” alisema.

Abiria mwingine, Nancy Leonard, alisema amelipa nauli ya Sh. 33,000 kwa mabasi yanayokwenda Arusha badala ya Sh. 25,000 ya bei elekezi iliyoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).   TIKETI MTANDAONI ZAKWAMA

Baadhi ya mawalaka walisema utaratibu wa tiketi mtandaoni unakwaza kwa sababu inachukua muda mrefu mmiliki wa gari kupata fedha.

Mmoja wa mawakala wa tiketi kwenda Moshi, Michael Mtemvu, alisema inachukua hadi wiki mbili kuingiziwa pesa zilizolipwa na abiria kupitia tiketi mtandao hali inayozorotesha utoaji huduma.

“Abiria anakata tiketi leo, anaondoka kesho, hela yake ndiyo tunaitegemea kujaza mafuta gari, kuifanyia marekebisho na kulipa ushuru. LATRA wanaingiza zile fedha baada ya wiki mbili, hela za kujiandaa tunapata wapi? Huo mfumo hatuoni kama una manufaa zaidi ya kutuumiza tu,” alisema.

Wakala mwingine, Godfrey Vincent, alisema licha ya huduma hiyo kuchelewesha mapato yao, pia bado mfumo wake haujatengemaa na kuwa kuna wakati mashine zinagoma kutoa risiti, hivyo kulazimika kurudi katika mfumo wa kawaida wa kutoa tiketi a mkono.

“Kuna wakati unatoa risiti kumi mashine inagoma kabisa kutoa tiketi, au inakwama kabisa mpaka uizime na kuiwasha, sasa inabidi turudi kwenye mfumo wa zamani, kwa kweli unakuwa ni usumbufu hasa kipindi hiki ambacho wasafiri ni wengi,” alisema.

Meneja wa mabasi ya Tashrif, Hamisi Shemweta, alisema changamoto nyingine ni kuwa abiria anauwezo wa kukata tiketi kwa siku za mbali jambo ambalo linaleta shida ikiwa gari alilokatiwa tiketi likapata hitilafu, tofauti na kama mteja angekata tiketi siku moja au mbili kabla ya kusafiri.

Aidha, aliwasihi abiria kuingia ndani na kukata tiketi kwenye ofisi zao moja kwa moja ili kuepuka madeiwaka wanaowawahi wakiwa barabarani na kuwaongezea kiwango cha nauli kwa manufaa yao binafsi huku lawama ikienda kwa mawakala hao.

LATRA YAFUNGUKA

Meneja Usalama na Mazingira wa LATRA, Geoffrey Silanda, alisema wameshatoa leseni za muda kwa magari 22 kutoka Dar es Saalam kwenda mikoani na magari 42 nchi nzima na kufanya jumla ya leseni za muda 64.

Alisema mchakato huo ulianza Desemba 8, mwaka huu, kwa kuzingatia mabasi yaliyotimiza masharti, ikiwamo kuwa na uwezo wa kubeba abiria wasiopungua 40, kuunganishwa kwenye mfumo wa tiketi mtandao na kuwa na leseni ya LATRA.

Aidha, alisema wameshafanyia kazi changamoto nyingi zinazoleta usumbufu kwa abiria ikiwamo huduma ya tiketi mtandao ambayo sasa wamiliki wanatapata zao moja kwa moja mara baada ya malipo hayo yanapifanyika kupitia benki husika.

Pia alisema vilevile wanashirikiana na Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) ambayo imekubali kuongeza behewa ambayo yatapachikwa kwenye treni za kwenda mikoani, ili kuongeza nguvu na kupunguza adha ya usafiri wanayopitia abiria kipindi hicho.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Abdallah Mohamed, alisema walifanya kikao na madereva wa mabasi na kuwasisitiza wafuate sheria za usalama barabarani na kanuni za LATRA ili kuwaepushia abiria usumbufu hasa msimu huu wa sikukuu.

“Tumewaambia mwaka huu hatutaki kusikia kabisa abiria wakilalamikia changamoto zilizosababishwa na wamiliki au mawakala, kila dereva ahakikishe anazingatia sheria, kabla magari hayajaondoka wahakikishe yapo salama, na pia abiria wote wakae kwenye siti, hakuna kusimamisha abiria,” alisema.

Chanzo: ippmedia.com