Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viziwi na changamoto ya wakalimani

31f5067ce39ed82047264899e79529e9 Viziwi na changamoto ya wakalimani

Thu, 14 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UZIWI ni ulemavu wa kukosa uwezo wa kusikia kwa ufasaha. Wapo watu huhusisha hali hiyo na ile ya kushindwa kuzungumza kwa ufasaha yaani bubu.

Lakini tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa wapo walio na aina hizo zote mbili za ulemavu kwa pamoja na pia wapo walio aina mojawapo, yaani uziwi lakini wanaweza kutamka maneno na wapo walio bubu lakini wanaweza kusikia japo kundi la walemavu wa namna hii lina watu wachache.

Kama ilivyo kwa makundi ya viziwi na bubu nayo yana mahitaji yake.

Ukiachilia mbali mahitaji muhimu anayopaswa kuyapata binadamu yeyote hapa duniani, kundi hili lina uhitaji maalumu wa kuwa na wakalimani ili kuwezesha mawasiliano kati ya watu wa kundi hilo na jamii inayowazunguka katika shughuli mbalimbali.

Mawasiliano baina ya kundi hili yanahitajika ili kuwawezesha wahusika kupata huduma za msingi katika nyanja mbalimbali ikiwemo huduma za matibabu, kibiashara, mikutano, upashanaji habari, masuala ya ibada na maeneo mengine kwa kuwa ni sehemu ya mambo yanayowahusu.

Hapa nchini kuna baadhi ya maeneo yamekwishafanya jitihada za uwepo wa wakalimani ili kuwezesha kundi hili kunufaika na huduma zinazotolewa katika eneo husika badala ya kuendelea kuwatenga.

Mwishoni mwa mwaka jana, Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ilisema inatarajia kutunga sera itakayozilazimu hospitali zote nchini kuwa na wakalimani wa lugha za alama ili kuwezesha watu wenye ulemavu wa kusikia kupatiwa huduma kwa urahisi kama wagonjwa wengine.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk Godwin Mollel alipenyeza hilo alipofanya ziara ya kikazi katika Hospitali za Rufaa za Kanda na Mkoa wa Mbeya zilizopo jijini Mbeya baada ya kupata taarifa ya uwepo wa mkalimani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.

Dk Mollel alisema katika utoaji wa huduma yapo makundi kadhaa yaliyosahaulika, hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo ni lazima kuwepo kwa sera ambayo itazilazimisha hospitali za umma kuwa na wataalamu wa lugha za alama.

“Walemavu wa kusikia wanahitaji huduma za afya kama ilivyo kwa watu wengine wanapohitaji huduma.

Lazima tuwe na sera itakayotuongoza kuhakikisha huduma hii inapatikana katika vituo vyetu vya kutolea huduma,” alisisitiza.

Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji alisema uongozi wa hospitali hiyo umeajiri mkalimani wa lugha ya alama ambapo mafanikio yaliyopatikana ni makubwa katika muda mfupi.

Dk Mbwanji alisema kwa kipindi cha muda mfupi zaidi ya watu 300 wasiosikia waliweza kujitokeza na kuanza kupata huduma katika hospitali hiyo baada ya kuwepo kwa mkalimani, jambo lililochangia na wao kuhamasika na kuanza kujitolea katika huduma mbalimbali.

Alisema kati ya hao 300 waliojitokeza, viziwi zaidi ya 70 walijikusanya na kujitolea damu kutokana na kuridhika na huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.

Anasema wengine walipimwa maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na kufanyiwa tohara, jambo ambalo huko nyuma liliwanyima fursa kutokana na ugumu wa mawasiliano.

Mafanikio haya yanaonesha uhalisia wa namna ukosefu wa wakalimani wa lugha za alama unavyokwamisha jamii ya watu wasio na usikivu kamilifu kushiriki katika mambo mbalimbali na muhimu ndani ya jamii zetu.

Ni dhahiri kuwa jitihada zaidi zinahitajika kuongeza kuhusu wakalimani katika maeneo yote yaliyo muhimu ikiwemo polisi, mahakamani, kwenye mikutano na kwingineko.

Desemba mwaka jana pia Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita) mkoa wa Mbeya kililiomba Baraza la Ushauri la watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini (TCRA-CCC) kuwaboreshea mifumo ya mawasiliano ili kuondokana na changamoto za kulazimika kutumia wakalimani.

Mwenyekiti wa Chavita mkoa, Tusa Mwalyego alitoa ombi hilo katika kikao cha wadau wa huduma za mawasiliano kilicholenga kutoa elimu na kuhamasisha umuhimu wa matumizi ya laini zilizosajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya taifa.

Tusa alisema kundi la viziwi limekuwa likisahaulika sana, hivyo ni vyema kupitia kikao hicho Serikali na wadau wakatambua changamoto zinazowakabili na kuona namna ya kutengeneza mfumo rasmi wa upatikanaji wa taarifa sahihi kwao.

“Sisi viziwi tunakumbana na changamoto nyingi katika mifumo ya mawasiliano… Kwa mfano natuma pesa nakosea, ninapohitaji maelekezo nalazimika kupiga simu huduma kwa wateja.

Sasa mimi sisikii bila ya kuwa na mkalimani. Hii ni changamoto,” anasema Tusa Mwenyekiti huyo pia alisema ufike wakati kundi hilo la viziwi kukumbukwa wakati wa mipango na mikakati yote ya Serikali kwa kuboresha masuala ya utandawazi hasa kuwashirikisha kwenye mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo.

Katika kikao hicho Katibu Mtendaji wa TCRA-CCC Mary Msuya, alisema ameichukua changamoto husika na kuahidi kuwa ataiwasilisha sehemu husika ili kuona namna ya kuliwezesha kundi hilo kunufaika na huduma za mawasiliano kama ilivyo kwa watu wengine.

“Kwenye mabaraza ya TCRA-CCC yanayoundwa katika kila mkoa kunakuwa na wajumbe wakiwemo mwakilishi kutoka kundi la walemavu ambaye huwakilisha watu wa aina zote za ulemavu lakini kwa changamoto hii iliyotolewa hapa ya wenzetu viziwi nitahakikisha ninaifikisha sehemu husika ili ifanyiwe kazi kwa kuwa wana haki ya kunufaika na huduma kama ilivyo kwa watu wengine,” anasisitiza Mary.

Harakati za viziwi katika kupambania haki zao hazijaishia hapo, maeneo mengi wanaonekana kuendelea kutoa kauli zaenye kulenga kuleta usawa kati yao na wanajamii wengine.

Januari 10 mwaka huu gazeti hili lilichapisha habari iliyopewa kichwa cha habari cha viziwi wataka ofisi za Serikali kuwa na mkalimani ikiandikwa na mwanahabari Mariam Juma kutoka Babati mkoani Manyara.

Katika habari hiyo Chavita mkoani Manyara kilishauri wawepo wakalimani katika ofisi za serikali na taasisi mbalimbali ili kuwarahisishia mawasiliano wanapofika kwaajili ya kufuata huduma mbalimbali.

Katibu wa Chavita mkoa wa Manyara, Anna Ngalawa alitoa ushauri huo kwenye warsha ya elimu ya kupambana na rushwa kwa viziwi iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).

Alisema mawasiliano ni changamoto kwa viziwi hivyo ipo haja ya kuwapo wakalimani ili wanapokwenda kwenye ofisi mbalimbali wapate mtu wa kuwasiliana, waelewane na wapate huduma wanazohitaji.

Anna alitoa mfano akisema wanapokwenda kupatiwa matibabu, mawasiliano huwa magumu hali inayosababisha kupatiwa huduma tofauti kutokana na daktari kutokuwa na uelewa mzuri wa lugha ya alama.

“Inakuwa ni hatari anaweza akampa kiziwi dawa ambayo haiendani na ugonjwa anaoumwa.” “Nimeamua kuwaleta hapa Takukuru waje tupatiwe elimu ya kupambana na rushwa kwa sababu mimi kama katibu wao wamekuwa wakiniletea malalamiko lakini sina uwezo wa kumaliza matatizo yao lakini wakipatiwa elimu hii watajua baadaye wakipata shida ya kuombwa rushwa yoyote wajue watakwenda wapi ili wasaidiwe,” alikaririwa Anna katika habari hiyo akisema.

Yapo maeneo mengi ambayo viziwi na mabubu wanahitaji msaada wa wakalimani ili waweze kupata huduma stahiki.

Ni wakati kwa wadau kushirikiana na serikali kutafuta ufumbuzi wa jambo ili ili kuleta usawa wa upatikanaji wa huduma ndani ya jamii ya watanzania.

Jambo muhimu kwa wadau ni kutambua kuwa hakuna aombae kuzaliwa ama kukutwa na ulemavu hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha usawa ndani ya jamii pasipo kujali ukamilifu au hali ya ulemavu uliopo kwa mwenzie.

Chanzo: habarileo.co.tz