Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viwe: Kwa vijana nimefanya vizuri nitaomba fursa UWT

56268 Pic+viwe

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Ni uchaguzi unaotarajiwa kushirikisha wanaume na wanawake Bara wa Tanzania na Zanzibar.

Wakati mwanga unaanza kujitokeza katika ushiriki wa wanawake, wanawake wa Zanzibar wanatajwa kuwa nyuma kujitokeza kugombania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia vyama vya siasa.

Ili kuondokana na hali hiyo, baadhi ya vijana wanasema wakati umefika wanawake kuamka. Mmoja wa vijana hao ni Viwe Ali Abdalla, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.

Katika mahojiano na gazeti hili, Viwe anasema haikuwa rahisi mpaka kushiriki na kuwa miongoni mwa wajumbe wa baraza la kutunga sheria Zanzibar, lakini alipiga moyo konde akawania nafasi hiyo na kushinda.

Alisema yapo mengi aliyopitia ikiwemo kuonekana hana uwezo wa kusimama mbele ya watu na kujielezea, lakini yote hayakuwahi kumkatisha tamaa bali aliyaweka pembeni na kusonga mbele.

Anasema wanawake wengi wana woga na wanakatishwa tamaa na watu ambao ni maadui kwao, lakini anaamini iwapo wanawake wataamka na kuhamasika, wataweza kushika nafasi nyingi za uongozi katika maeneo mbalimbali.

Kwa sababu ya wingi wa wanawake, bila shaka wao ndio wanaongeza idadi kubwa ya wapiga kura na iwapo watashikamana na kuacha tofauti baina yao, bila shaka wataingiza wenzao wengi kwenye uongozi.

Akizungumzia changamoto ambazo amekutana nazo na anaamini wanakutana nazo wanawake wengine, Viwe anasema ni pamoja na utayari wa wanawake wenyewe kushiriki kinyanganyiro cha siasa.

Anasema kuna mazingira ambayo yanawarudisha wanawake wengi nyuma na kubaki ndoto za kuwa viongozi bila kutimia.

Ili kuepuka hali hiyo, Viwe anawataka wanawake wenzake kutokata tamaa na maneno hayo badala yake wachukue changamoto hizo kuzifanya fursa za kusonga mbele na kujiwekea matumaini ya kushinda.

Akizungumzia namna gani amewasaidia wanawake wenzake, hususani vijana, kwa kipindi ambacho amekuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi alisema ni mambo mbalimbali ambayo ameshiriki kama kiongozi.

Anasema amekuwa akiandaa mijadala mbalimbali yenye lengo la kuwanoa wanawake ili waweze kuona umuhimu wa kushiriki siasa na kugombea nafasi za uongozi.

Kuhusu nini nafasi yake kama kijana katika Baraza la Wawakilishi, anasema awali alipata shida kwa kutokana na ugeni aliokuwa nao lakini haikumchukua muda aliizoea hali hiyo baada ya kupewa mafunzo maalumu na sasa amekua kinara wa kuchangia hoja na miswada mbalimbali.



Chanzo: mwananchi.co.tz