Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viwanda matatani kwa dawa za kulevya

15740 Pic+viwanda TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema imebaini baadhi ya viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu nchini huchepusha kemikali kwa lengo la kugengeneza dawa za kulevya.

DCEA imesema viwanda hivyo vinachepusha hususan kemikali aina ya Pseudo-Ephedrine ambayo ni kiambato muhimu katika kutengeneza baadhi ya dawa za binadamu na kuitumia kutengeneza heroin na cocaine katika maabara za vichochoroni.

Kamishna wa Ukaguzi na Sayansi Jinai wa DCEA, Bertha Mamuya amesema kugundulika kwa ujanja huo kumetokana na operesheni waliyofanya nchi nzima kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Alisema waliamua kufanya operasheni hiyo ili kujiridhisha kama kila kiwanda kinachoagiza kemikali hiyo nchini huitumia kwa matumizi halisi kama walivyoiagiza.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mamuya alisema wamebaini baadhi ya viwanda vimekuwa vikipunguza kiwango halisi cha kemikali hiyo kinachotakiwa kutumika watengenezapo dawa husika za binadamu na kuchepusha inayobaki kwa matumizi haramu.

“Tuligundua kuwa kuna baadhi ya viwanda vya dawa za binadamu walioagiza kemikali hiyo kwa ajili ya kutengeneza dawa ya binadamu wanaiondoa au kuipunguza katika mchanganyiko wa dawa na matokeo yake, dawa inayotengenezwa inakuwa chini ya kiwango.

“Kemikali aina ya Pseudo-Ephedrine huiagiza kwa ajili ya kutengeneza dawa za binadamu, lakini baadhi ya wenye viwanda hawaitumii na kinachotokea ni kwamba, dawa husika hutengenezwa chini ya kiwango kinachotakiwa. Wasiwasi wetu ni kuwa kemikali hiyo hutumika kutengenezea dawa za kulevya,” alisema Mamuya.

Alisema kwa kushirikiana na TFDA walikamata chupa 500 za dawa za tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine ambazo zinasimamiwa kwa utaratibu maalumu duniani baada ya kuingizwa kiholela nchini kupita mpaka wa Sirari, Mara.

Alisema dawa hizo zinatumika kwa matumizi ya hospitali pekee na zinapohitajika, hospitali husika hutakiwa kuomba kibali TFDA ambayo huiagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

“Cha kushangaza mtu anavuka mpakani akiwa na dawa za Pethidine ambazo wanazitumia kutengenezea dawa za kulevya,” alisema.

Mamuya alisema, “Utakuta mtu anakutwa akiwa na vidonge zaidi ya 200 bila ya kuwa na kibali maalumu wanazitumia kutengeneza dawa za kulevya.”

Alitolea mfano wa dawa hizo kuwa ni aina ya Ritalin, Nootropil, Xanax, Promethazine, Ketamax, Codein Phosphate, Rohypnol na Pethidine.

Mamuya alisema kuanzia Julai 17, 2017 hadi Juni 18 mwaka huu, wamekamata kemikali bashirifu ya kimiminika lita 304,515, kemikali bashirifu mfumo wa unga kilo 22,034 na wamezuia kemikali bashirifu tani 12,052.

Hata hivyo, alisema tatizo la kemikali si la Tanzania tu, bali la nchi mbalimbali, “Hivyo tunatumia mifumo ya kielektroniki ambayo inafuatilia jinsi kemikali bashirifu inavyosafirishwa kabla haijaingizwa nchini na kwa kibali maalumu. Itafuatiliwa na kuzuiwa kabla ya kuingia nchini.”

Ofisa Habari wa TFDA, Gaudencia Simwanza alisema jana kuwa kuna kemikali zinazotumika kutengeneza dawa ambazo zina viambato vya dawa za kulevya lakini mamlaka hiyo imekuwa ikidhibiti matumizi yake kwa kuitaka kila hospitali kuomba kibali cha matumizi ya dawa hizo.

“Dawa zote zinazotumika kwa nusu kaputi na nyingine zenye viambata vya dawa za kulevya lazima ziombewe vibali kila zinapotakiwa na hospitali fulani na hata kabla ya kutolewa kwa kibali kingine ni lazima kuwepo na matumizi ya kibali kilichopita,” alisema Simwanza.

Alisema TFDA inafanya hivyo kwa sababu dawa hizo zipo chini ya udhibiti wake na kutokana na unyeti wake na madhara yake endapo hazitatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali haikuwa tayari kuzungumzia suala hilo jana huku msemaji wake, Sylvester Omari akimtaka kutafuta habari zaidi kutoka DCEA.

Chanzo: mwananchi.co.tz