Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viungo vya maiti vyakatwa, makaburi yavunjwa

Kab Viungo vya maiti vyakatwa, makaburi yavunjwa

Tue, 1 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wasiojulikana wamevamia makaburi ya Serikali Wilayani Magu Mkoani Mwanza na kuvunja majeneza huku wakikata baadhi ya viungo vya maiti na kundoka navyo.

Kadhalika, katika uvamizi huo watu hao wamedaiwa kuvunja makaburi yaliyojengwa kwa kutumia zege kisha kuchukua nondo na misalaba ya chuma kwa lengo la kwenda kuviuza kama vyuma chakavu.

Hatua hiyo imeiweka serikali wilayani humo katika tahadhari na kuagiza ufanyike msako ili kuwabaini wanaofanya vitendo hivyo vya kiovu.

Tayari serikali imelaani na kukemea vitendo ambavyo imeviita vya kikatili na visivyokuwa vya kawaida katika tamaduni za kitanzania.

Kutokana na vitendo hivyo, watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa mahakamani huku msako ukiendelea ili kuwabaini wengine wanaodaiwa kufanya uhalifu huo.

Ofisa Habari wa Wilaya ya Magu, Pascaly Mashamba, ameiambia Nipashe kwamba watu hao walikamatwa hivi karibuni kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo hivyo vya kikatili vya kubomoa makaburi.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali, amekiri kuwapo kwa vitendo hivyo, baada ya kutembelea eneo hilo akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.

Alisema uchunguzi wa awali umebaini waliofanya tukio hilo la kinyama ni watu wanaotafuta nondo na misalaba kwa lengo la kwenda kuviuza kama vyuma chakavu.

Wakati mkuu huyo wa wilaya akitoa onyo hilo, kumebainika pia watu hao walivunja majeneza na kukata baadhi ya viungo vya maiti na kuondoka navyo.

Kwa takribani wiki moja sasa, mkuu huyo wa wilaya, aliagiza ufanyike msako ili kuwabaini watu wanaofanya vitendo hivyo vya kikatili.

Akizungumza na Nipashe, Kali alisema msako wa kuwasaka watu hao umeanza na ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi hiyo usiku na mchana ili kuendelea kuwabaini watuhumiwa hao.

Alisema alipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu kuwapo uvunjaji wa makaburi hayo na kwamba alifika huko haraka na kukuta makaburi yaliyovunjwa yakiwa wazi.

Alisema watu hao wanavunja misalaba iliyotengenezwa kwa nondo pamoja na kubomoa zege la juu kisha kuchomoa nondo zote.

Kali akiwa katika ziara ya kuhamisha matumizi ya anwani ya makazi katika eneo hilo, alisema, ni lazima watu hao wakamatwe ili iwe fundisho kwa wengine.

Kutokana na hali hiyo, kwa sasa umeimarishwa ulinzi wa mgambo ambao wameagizwa kulinda makaburi hayo wakati ndugu wa marehemu waliozikwa hapo wakifanya utaratibu wa kuyajengea upya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live