Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vituo vya kilimo kuanzishwa kila halmashauri

145f6be1627a9fdf096da312c1a00e76 Vituo vya kilimo kuanzishwa kila halmashauri

Sun, 14 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo imekuja na mpango wa kuanzisha vituo vya kilimo katika kila halmashauri ya wilaya pamoja na kutoa pikipiki kwa maofisa ugani wote nchini zitakazowekewa GPS kwa lengo la kuboresha zaidi sekta hiyo ya kilimo.

Vituo hivyo vya kilimo pamoja na mambo mengine vitakuwa na vifaa vya kisasa vya kimaabara pamoja na kuwa na maabara inayotembea itakayotumika kupima afya ya udongo bure na hivyo kumshauri mkulima juu ya aina ya udongo alionao tiba yake na zao gani apande.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyasema hayo bungeni Dodoma jana wakati akichangia hoja ya mipango ya kitaifa ya maendeleo ya muda mfupi na mrefu iliyowasilishwa bungeni hapo na Waziri wa Katiba na Sheria Dk Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Mipango hiyo ni pamoja na Mpango wa Kitaifa na mwongozo wa bajeti kwa mwaka 2021/22 na Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26.

“Katika mjadala huu, wabunge wamechangia sana suala la udongo, suala la ugani na suala la mbegu hasa za mafuta. Sasa kuhusu suala la ugani na suala la kupima afya ya udongo, wizara tutakuja na mpango katika bajeti ijayo, wa kuanzisha agriculture Centre (kituo) katika kila halmashauri,” alieleza Bashe.

Alisema katika hatua ya pili, katika vituo hivyo vya kilimo pia, watagawa pikipiki 700,000 kwa maofisa ugani wa nchi nzima katika msimu ujao na kila pikipiki itafungwa GPS na kuongeza kuwa sasa wameanzisha kituo cha huduma katika Wizara ya Kilimo ambacho kupitian GPS hizo kitakuwa kinafuatilia maofisa ugani hao ili kujua kama ofisa ugani anafanya kazi katika eneo lake.

Alisema kuhusu suala maendeleo na utafiti pamoja na mbegu, wizara hiyo imeamua kuwa suala la utafiti na maendelea hakuna tena kutegemea fedha za ufadhili.

Aliongeza kuwa pia wamebadili mfumo na wameanza na majaribio katika zao la pamba na wanatarajia kufanya majaribio pia katika zao la korosho msimu ujao na kuwa katika jaribio la pamba, mwaka huu, wamegawia wakulima mbegu na dawa bure ambazo wamezipata kutokana na mjengeko wa bei.

Kuhusu zao la chai alisema serikali imeamua kuanza na mchakato wa kuweka soko la chai jijini Dar es Salaam, ambalo litakuwa ni kwa ajili ya kuuza zao la chai moja kwa moja lakini vilevile kiwanda cha mponde nacho kitafunguliwa.

Aidha, alisema mwaka huu wamepanga korosho zote zitasafirishwa kwa kutumia gunia za katani.

“Na nitumie Bunge hili kumuambia mwekezaji ambaye ana viwanda viwili vya magunia cha Morogoro na Kilimanjaro tunampa kazi akishindwa tutapeleka mapendekezo serikalini kumnyang'anya viwanda hivi tuwape wawekezaji wengine,” alisema.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angelina Mabula alikiri kuwa mpaka sasa serikali imepima asilimia 25 tu ya ardhi nchi nzima na asilimia 75 haijafikiwa.

Alisema katika hizo asilimia 25 zilizopimwa jumla ya maeneo ya viwanda 2,346 na zaidi ya mashamba 23,000 yamepimwa na kusisitiza kuwa wizara hiyo inajipanga kuhakikisha ardhi yote inapimwa.

Chanzo: habarileo.co.tz