Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mjini James Kaji amesema Wasafirishaji wa Huduma za Bodaboda pamoja na Bajaji wataanza kutumia vituo vinavyotambulika kwa namba sambamba na kuvaa Kiakisi (Reflector) zenye namba watakazokuwa wanatumia pindi wanapokuwa Barabarani ili kupunguza uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza kwa baadhi ya Vijana ambao wamekuwa wakifanya uhalifu kwa kutumia Bodaboda na Bajaji kushindwa kutambulika.
DC Kaji amesema hayo wakati akihitimisha kikao na Madiwani wa Jiji la Tanga ambapo amesema wamekubaliana na Uongozi wa Bodaboda na Bajaji Jijini Tanga kutambulika kwa namba pamoja na vituo vyao ili inapotokea uhalifu au abiria kusahau mzigo, Bajaji na Bodaboda hiyo iweze kutambulika kwa haraka pamoja na kulinda usalama tofauti na sasa ambapo hazina utambulisho wowote.
Amesema utekelezaji huo utaanza mara moja ambapo atakutana tena na Uongozi wa Bodaboda na Bajaji ambao tayari wamekamilisha mchakato wa katiba kwa ajili ya kuanza kwa utekelezaji huo.