Katika kuboresha huduma kwa wagonjwa, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeongeza idadi ya viti ‘vitanda’ vya huduma za meno na vitanda vya kujifungulia katika vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
Kufungwa kwa vitanda hivyo kutaondoa foleni iliyokuwepo awali, ambapo wagonjwa waliohitaji huduma ya meno walilazimika kukaa foleni ya muda mrefu kutokana na kuwepo kwa kitanda kimoja pekee.
Akizungumza na Mwananchi, Novemba 17, 2023 wakati akipokea shehena ya vitanda na dawa kutoka MSD, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Cyprian Mhagama amesema ujio wa vitanda hivyo utaboresha huduma.
“Vitanda hivi vitaboresha huduma za matibabu ya meno, awali kila kituo kilikuwa na kitanda kimoja pekee kwa sasa tutaweza kuwahudumia wateja wawili kwa wakati mmoja kwa maana huduma zetu zitakwenda kubadilika na wateja hawatasubiri kwa muda mrefu huduma,” amesema.
Mhagama ambaye pia ni Muuguzi Mkuu wa wilaya amesema wamepokea pia kitanda cha kujifungulia kwa ajili ya kituo cha afya Mundindi, ambapo hapo awali walikuwa navyo vichache kwa hiyo kwa sasa kinamama wengi wataweza kujifungua kwa wakati mmoja.
“Vifaa vimegawanywa kulingana na mahitaji, kuna vitanda kwa ajili ya huduma za meno, kimoja Hospitali ya Wilaya ya Ludewa kingine kituo cha afya Luwilo ambako nako walikuwa na kitanda kimoja, tumepokea vitanda vingine vya wagonjwa vya kituo hichohicho,” amesema.
Mkazi wa Ludewa, Oliva Nziku ameishkuru Serikali kuongeza vifaa tiba hivyo kwa ajili ya huduma za meno kwani foleni ilikuwa kubwa.
“Tulikuwa na uhaba Hospitali ya Ludewa, tulikuwa na kitanda kimoja pekee ukija kutibiwa jino waganga wapo lakini kitanda ni kimoja inabidi ukae foleni, naamini sasa tukihudumiwa wawili kwa wakati mmoja itasaidia kupunguza foleni iliyokuwepo awali,” amesema Nziku.
Mfamasia wa Halmashauri ya Ludewa, Christina Kilwale amesema kwa sasa upatikanaji wa dawa katika eneo hilo ni asilimia 94 na imepanda kutokana na upatikanaji mkubwa uliopo katika bohari ya Kanda ya Iringa kwa kuwa dawa asilimia kubwa zikiagizwa zinapatikana kwa muda muafaka.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni kupokea dawa kila baada ya miezi miwili, ikilinganishwa na hapo nyuma kwa mwaka walipokea mara nne.
“Hii inaleta furaha kwamba unapoletewa dawa zinakuwa hasijaisha, tayari unapokea nyingine. Zamani ukiagiza dawa 100 unaletewa hata 20 lakini kwa sasa ukiagiza 100 unaletewa 80 idadi imepanda kiasi ulichokosa kinakuwa kidogo ukilinganisha na kile ulichopokea,” amesema Kilwale.
Mfamasia huyo ameongeza kuwa hiyo imesaidia kupunguza vituo kuagiza dawa kwa washitiri ambao hutoza bei kubwa ya dawa hivyo vituo hupata unafuu wanapopokea dawa kutoka MSD.