Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vitabu vya kiada milioni 30/vyawasilishwa sekondari Nyasa

023ca26c3ded0d85eeff816fb85f24b0.png Vitabu vya kiada milioni 30/vyawasilishwa sekondari Nyasa

Sun, 18 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI wilayani Nyasa, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania, imekabidhi vitabu 712 vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 30 kwa Shule ya Sekondari Mbamba bay ili kutatua changamoto ya upungufu wa vitabu vya masomo mbalimbali.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba alikabidhi vitabu hivyo jana katika Ukumbi wa Kassim Majaliwa uliopo katika Shule ya Sekondari Mbamba Bay, wilayani hapa na kumpongeza Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Mwalimu Rogers Semwalekwa kwa kufanya ufuatiliaji katika shule zote za sekondari wilayani humo na kubaini changamoto mbalimbali zilizopo katika shule, na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.

Chilumba aliongeza kuwa Semwalekwa ni mfano wa kuigwa na walimu, wafanyakazi wengine, Wakuu wa Idara zingine kwa kuwa amekuwa mbunifu wa kuzifuatilia shule zake, kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitatua kwa haraka kwa kutumia ubunifu wake wa kwenda Taasisi ya Elimu Tanzania na kupatiwa vitabu hivyo.

Aidha alitoa wito kwa wakuu wa idara na vitengo wilayani hapa, kuwa wabunifu na kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na kuyapatia ufumbuzi.

Awali Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbamba Bay, Mwalimu Zawadi Msambwa akitoa taarifa fupi Kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, alisema kupatikana kwa vitabu hivyo kutawaongezea wanafunzi ari ya kujifunza kwa kuwa awali

kulikuwa na upungufu wa vitabu hasa vya kidato cha Tano na Sita, kwa hiyo wanaishukuru Taasisi ya Elimu Tanzania na Ofisa Elimu Sekondari Nyasa kwa juhudi zake za kutatua changamoto katikashule zake. Aidha alivitaja vitabu alivyopokea kuwa ni vitabu vya Kemia, Bayolojia, Kiswahili na Hisabati.

Ofisa Elimu Sekondari Wilayani hapa aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu mitihani, na kuahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali katika shule zote wilayani Nyasa ili waweze kupata elibu bora.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, wilaya ya Nyasa Eiphrem Kawonga alimpongeza Ofisa Elimu huyo na kumtaka aendelee na juhudi hizo za kutatua changamoto zinazoikabili Idara ya Elimu Sekondari kama alivyofanya.

Kwa upande wao, wanafunzi wa sekondari Mbamba bay wameipongeza serikali kwa kutatua changamoto mbalimbali katika shule yao na kuahidi kusoma kwa bidii na kuitangaza vema shule hiyo kwa kutoa elimu bora na kuwaandaa wanafunzi katika soko la ushindani wa elimu na ajira.

Chanzo: www.habarileo.co.tz