Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Visima Kimbiji kuwanufaisha wananchi Kigamboni

Mradikigambonipic Visima Kimbiji kuwanufaisha wananchi Kigamboni

Tue, 16 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mradi wa visima vya maji Kimbiji utakaozalisha lita 57 milioni kwa siku unatarajia kukamilika Aprili 2022 ambapo visima saba kati ya 12 vimekamilika.

Mradi huo utakuwa na tanki lenye uwezi wa kuhifadhi lita 15 milioni unaelezwa kuwa utamaliza adha ya maji katika eneo la Kigambo jijini Dar es Salaam.

Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) leo Jumanne Novemba 16, 2021 imetembelea mradi huo uliofikia asilimia 50 ya ujenzi.

Ziara hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuelekeza kuangaliwa kwa vyanzo vingine vya maji ili kukabiliana na changamoto ya nishati hiyo.

Mkurugenzi wa Uwekezaji na Miradi wa Dawasa, Mhandisi Ramadhan Mtindasi amesema mradi huo uliopaswa kukamilia Novemba mwaka huu, utakamilika Aprili mwakani.

Amesema kuchelewa huko kumetokana na changamoto kadhaa ikiwemo janga la Uviko 19 lililochangia kuchelewa kwa vifaa muhimu ambavyo mkandarasi aliviagiza kutoka nje.

“Changamoto ya vifaa tayari imeshapatiwa ufumbuzi kuna ambavyo tayari vimeshawasili vingine viko njiani na kazi inaendelea tuna imani kufikia Aprili mradi utakuwa umekamilika tayari kwa kuanza kuhudumia wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani,”.

Amesema katika mipango ya baadaye mradi huo pia utahusisha utengenezaji wa bomba kubwa ambalo litapita baharini likichukua maji na kuyapeleka maeneo ya katikati ya jiji ili kupunguza utegemezi wa Ruvu chini.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Mwenyekiti wa bodi ya Dawasa, Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

“Niwaombe wakandarasi waongeze kasi, wasizembee na yasijitokeze mambo ya visingizio, shida ya maji eneo la Kigamboni ni ya muda mrefu tunataka mradi huu ukamilike ukamalize shida hiyo.

“Kuhusu changamoto za fedha na nyingine ambazo zinatuhusu upande wa Dawasa tumezichukua tunakwenda kuzifanyia kazi ili kuhakikisha mradi huu unamalizika kwa wakati au hata kabla ya wakati,” amesema Jenerali mstaafu Mwamunyange.

Chanzo: mwananchidigital