Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wazima vurugu Tunduma

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tunduma. Viongozi wa Serikali nchini Tanzania na Zambia leo Jumapili Machi 24, 2019 wamezima vurugu za vijana katika mpaka wa Tunduma wakishinikiza kuachiwa kwa Wazambia 15 waliokuwa wakishirikiliwa na polisi nchini.

Watu hao walikamatwa baada ya polisi kufanya msako wa kukamata wahalifu.

Akizungumza leo, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando amesema tukio hilo limehusisha watu wachache walioanza kuandamana katika mpaka huo wa nchi hizo mbili wakishinikiza waliokamatwa kuachiwa.

Amesema kufuatia hali hiyo, kamati ya ulinzi ya pande zote mbili zilikutana na kukubaliana kushughulikia jambo hilo kwa pamoja.

“Hatujawaachia huru kwa sababu operesheni yetu tulishirikiana na wenzetu wa Zambia, hivyo watashtakiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo pande zote mbili,” amesema Irando.

Meneja wa forodha katika mpaka wa Tunduma, Johnmather Sirro amesema sakata hilo limetokana na baadhi ya watu kutoa taarifa potofu huku baadhi wakiwatisha waliokuwa wakiingia nchini na kusababisha shughuli mbalimbali katika mpaka huo kusimama.

Amesema shughuli za kupitisha magari zilisitishwa kwa muda baadaye kurejea katika hali ya kawaida.

Mmoja wa wafanyabiashara katika mpaka huo, Kim Mwakasege amesema jambo hilo linapaswa kutazamwa kwa kina.

Amesema kuna madai kuwa siku za hivi karibuni baadhi ya watu waliporwa fedha na watu waliojitambulisha kuwa ni askari kutoka nchi jirani.

Elina Sichula amesema vurugu hizo zimetokana na raia wa Zambia kurusha mawe upande wa Tanzania huku Sadick Lauden akibainisha kuwa kitendo hicho kilihatarisha amani.

“Kukamatwa kwa watu wanaodaiwa kuwa wahalifu ni jambo la kawaida ni kuacha tu sheria zichukue mkondo wake,” amesema Lauden.



Chanzo: mwananchi.co.tz