Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wapya Shirecu waonywa

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wapya wa Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (Shirecu) wajipime kama wako tayari kuwatumikia wananchi na kama sivyo waachie ngazi.

Ametoa onyo hilo jana Ijumaa, Julai 13, 2018 wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani mara baada ya kukagua soko la pamba kwenye kijiji hicho, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo, amewataka wajumbe hao wajitafakari upya na kujihoji kama wameomba vyeo hivyo kwa ajili ya kupata utajiri ama kuwatumikia wananchi.

“Napenda kusisitiza kwamba ule mfumo wa zamani wa ushirika hivi sasa haupo. Kama uliomba cheo hicho kwa ajili ya kupata utajiri, ni bora ujiondoe sasa hivi, njoo uniambie wakati bado niko kwenye ziara ya mkoa huu, tutatafuta wajumbe wengine ambao ni waaminifu,” amesema.

“Nasisitiza kwa viongozi wa AMCOS na wa SHIRECU, mmeomba vyeo hivyo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na siyo kujinufaisha binafsi.”

Amesema tofauti na ilivyokuwa awali, Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuona ushirika wa sasa ukirejesha matumaini kwa wananchi.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema zamani, ushirika ulimwezesha mwananchi kununua baiskeli au redio lakini kutokana na hali ilivyobadilika, jambo hilo lilikuwa haliwezekani.

“Tunataka ushirika wa sasa ubadilike na umwezeshe mwananchi kununua gari la kutembelea ama kujenga nyumba bora,” amesema.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz