Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa vijiji wapiga pesa za wahamiaji haramu

29001 Viongozi+pic TanzaniaWeb

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Biashara ya wahamiaji haramu kutoka Somalia na Ethiopia, inatajwa kuchangiwa na dau linalofikia Dola 5,000 sawa na Sh11 milioni linalotolewa kwa washiriki wa biashara hiyo.

Wakati hilo likibainika, Idara ya Uhamiaji Kilimanjaro, imesema tayari imebaini mawakala 35 ambao mawasiliano yao yanachunguzwa ili kubaini mtandao wote na kuutokomeza.

Baadhi ya viongozi wa vijiji, vitongoji na mgambo zaidi ya 10 katika wilaya mbili za Mwanga na Moshi, vinavyopakana na nchi ya Kenya, wanatajwa kugeuza wahamiaji haramu kuwa mtaji.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kila mhamiaji hulipa kati ya Sh100,000 na Sh200,000 ili kuhifadhiwa katika nyumba za wenyeji wakati mawakala wakiwatafutia usafiri kwenda Mbeya.

Wakati kundi hilo likitajwa kuwa sehemu ya mtandao unaofanikisha kupokelewa, kuhifadhiwa na kusafirishwa kwa wahamiaji haramu, baadhi ya vigogo wa polisi wametajwa kuwa sehemu ya mtandao.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa wiki mbili, inadaiwa mawakala wakubwa wa biashara hiyo wapo Somalia na Kenya, na kila mhamiaji hulipa kati ya Dola 3,000 na 5,000 za Marekani.

Fedha hizo ni kwa ajili ya usafiri kutoka Somalia hadi Kenya na baadae kutoka vijiji vya mpakani mwa Tanzania na Kenya, hadi mkoani Mbeya na baadae kuvuka mpaka kwenda Afrika Kusini.

Vijiji vya Tanzania vinavyotajwa kutumika kama uchochoro wa kuwapitisha wahamiaji hao ni Kitobo, Holili na Tarakea wilayani Rombo na Madarasani, Kitobo na Riata wilayani Moshi.

Wilayani Mwanga, vijiji vilivyopo kata za Kileo, Kivisini, Jipe na Toloha, baadhi ya viongozi wa vijiji, vitongoji na mgambo wanahusishwa kusaidia biashara hiyo.

Ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi wilayani Mwanga (jina tunalo), anatajwa na vyombo vya usalama kuwa miongoni mwa polisi wanaojihusisha kusafirisha wahamiaji wa Ethiopia na Somalia. Mkazi mmoja wa eneo la Mariatabu mpakani mwa Kenya na Tanzania, alidokeza kuwa waendesha pikipiki (bodaboda), hulipwa Sh50,000 kwa kichwa kuwavusha toka Taveta kuja Tanzania.

“Kutoka hapa kwenda pori la Chekereni wanachukuliwa na bodaboda, kila kichwa ni Sh50,000. Wanajificha hapo hadi wanapopatiwa usafiri barabara kuu ya Moshi-Dar es Salaam,”alidai.

“Kuna wanaohifadhiwa kwenye vijiji pale Chekereni na wanavuna pesa, kwa sababu si kuhifadhi tu na kuwahudumia chakula. Kila siku kwa kila kichwa si chini ya Sh100,000,”alieleza.

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Kileo ambaye hakutaka jina lake litajwe akihofia kulipiziwa kisasi, alidai hakuna wahamiaji haramu kwa makundi wanaweza kuhifadhiwa bila viongozi kufahamu.

Uhamiaji wabaini mawakala 35

Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Albert Rwelamira, alikiri wilaya za maeneo ya Mwanga na Moshi, kutumika kupokea na kuhifadhi wahamiaji haramu na tayari wamebaini uwapo wa mawakala 35 wanaohusika kupokea na kusafirisha wahamiaji hao.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Kilmanjaro, Hamis Issah alipoulizwa alisema hana taarifa hizo wakati mkuu wa wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho alisema tatizo hilo lipo na wamekuwa wakifanya kila njia kuwabaini.

kwamba wako maeneo mengi na si mpakani pekee.

Rwelamira alisema tayari wametambua majina na mawasiliano ya simu ya mawakala hao na kwamba kwa sasa hawawezi kuwataja kwa kuwa bado kuna uchunguzi yakiwamo mawasiliano unaendelea.

“Katika hao ambao tumewabaini huenda wakawepo viongozi wa vijiji, mitaa, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida kwa kuwa kinachotambulika wapo watanzania wanaowasaidia,”alisema.

Mkuu huyo alieleza kuwa katika wilaya ya Mwanga waneshakamata wahamiaji haramu zaidi ya mara tatu hivyo kunaweza kuwepo watu au mawakala wanaohusika kusafirisha na kuhifadhi watu hao.

“Watu hawa wanapoingia nchini, mara nyingi husafirishwa kwa bodaboda, na kawaida haiwei kubeba watu zaidi ya watatu,hivyo huchukuliwa mmoja au wawili na kuhifadhiwa mahali,”alisema.

“Ikifika shehena ya kutosha ndio wanapakiwa hivyo wanaweza kuhifadhiwa Mwanga, Moshi au Rombo lakini nataka niwaonye wanaofanya hili wajue siku zao zinahesabika,”alisema Rwelamira.

Mkuu huyo wa Uhamiaji alitahadharisha wamiliki wa vyombo vya usafiri yakiwamo magari na pikipiki yanayotumika kuwasafirisha na wamiliki wa nyumba, kuwa mali zao zitataifishwa wakikamatwa.

Akitoa takwimu, Rwelamira alisema katika kipindi cha Januari hadi Novemba 22,2018, Wahamiaji haramu 60 raia wa Ethiopia wamekamatwa kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume cha sheria.

Mbali na hao, watu wengine 43 Raia wa nchi jirani ya Kenya wenye asili ya Somalia, walizuiwa mpakani wakati wakitaka kuingia nchini kinyume cha sheria.

“Raia wa Ethiopia 60 walikamatwa baada ya kuingia nchini bila ya kuwa na hati za kusafiria tulizuia watu 43 wenye asili ya Somalia wakiwa bado mpakani upande wa Kenya wakitaka kuvuka”alisema.

RPC Kilimanjaro, DC wazungumza

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah, alipoulizwa juu ya uwepo wa biashara ya wahamiaji haramu na uwepo wa mitandao inayonufaika na biashara hiyo alisema hana taarifa hizo.

Kwa mujibu wa Kamanda Issah, taarifa za aina hiyo zinahitaji uchunguzi wa kina kabla ya kuzitolea taarifa, lakini akaahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa uzito unaostahili ili kubaini ukweli.

Kamanda Issah alisema wahalifu siku zote wanaishi na jamii huko mitaani, hivyo Jamii isipotoa ushirikiano kwa polisi kwa kufichua maovu, polisi peke yao hawawezi kuwabaini wahalifu hao.

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho, alisema tatizo la baadhi ya wananchi katika wilaya yake kuhifadhi wahamiaji haramu lipo na wamekuwa wakifanya kila njia kuwabaini.

“Hizo kata nne unazosema (Kileo, Kivisini, Jipe na Toloha) zimepakana na Kenya. Kwa mfano hapo Ziwa Jipe kuna madai baadhi ya wahamiaji huingia nchini kwa kutumia mitumbwi,”alieleza.

“Mwishoni mwa mwezi wa Septemba kama sijakosea tulikamata vijana (wahamiaji haramu) 19 kwenye kijiji cha Mnoa. Lakini niseme jambo moja, tangu nimekuja hapa ninakula nao sahani moja”.

Hata hivyo alisema, lipo tatizo katika wilaya yake kwake kwamba hakuna ofisi ya Uhamiaji na hicho ni kikwazo katika kudhibiti biashara hiyo, lakini akasema wanakamilisha mchakato ofisi hiyo iwepo.

“Mkakati mwingine nilionao ni kuwa sasa hivi tukiwakamata tunawaswaga kuwarudisha walipoingilia. Hatutaki baadae tutumie gharama zetu na ndege zetu kuwarudishwa walikotoka,”alisisitiza.

Mbogho aliiomba Idara ya Uhamiaji kama katika majina 35 ya mawakala waliowabaini wapo wanaoishi katika wilaya yake, wampatie majina ili aanze kushughulika nao kwa mujibu wa sheria.

Adhabu kwa wanaohifadhi ikoje?

Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Albert Msando, alisema adhabu zinazohusiana na makosa ya wahamiaji haramu huanzia faini hadi kifungo kulingana na kosa ambalo mtu anashitakiwa nalo.

“Wengi unakuta anashitakiwa yeye mwenyewe kama mhamiaji lakini kuna makosa mengine kama ya kumhifadhi, kufadhili hiyo biashara na kuwasafirisha ambayo huwaangukia Watanzania,”alisema.

Sheria Usafirishaji Binadamu ya mwaka 2008, kifungu cha 4, imetoa adhabu ya kati ya Sh5 milioni na Sh100 milioni au kifungu cha miaka saba jela, kwa mtu anayesafirisha au kuhifadhi mhamiaji haramu.

Wakili Msando alisema sheria pia imetoa adhabu ya kutaifishwa kwa chombo cha usafiri kilichotumika katika kusafirisha wahamiaji haramu na pia kutaifishwa kwa nyumba iliyotumika kuwahifadhi.



Chanzo: mwananchi.co.tz