Baadhi ya Walimu ambao ni Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Njombe wamemuomba Rais wa Chama hicho Leah Ulaya pamoja na Katibu wa CWT Taifa Japhet Maganga kujitokeza na kuwaeleza Watanzania sababu zilizowafanya kukataa uteuzi wa Ukuu wa Wilaya uliofanywa na Rais Dkt. Samia January mwaka huu na kwamba Ualimu unalipa kiasi gani hadi wakatae uteuzi huo.
Mjumbe wa Kamati Tendaji (CWT) - Taifa kutoka Mkoa wa Njombe , Thobias Sanga kwa niaba ya Walimu amesema Chama hicho kwa sasa kimekosa mahusiano mazuri na Serikali kutokana na changamoto nyingi ikiwemo Viongozi wao wa juu kutokubali uteuzi waliopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu zisizojulikana na kuleta taharuki kwa Walimu.
"Tumekuwa tukipata wakati mgumu kuwaongoza Walimu na tukipita maofisi mabalimbali kupata huduma tumekuwa tukiulizwa kwanini mnakataa uteuzi wa Rais, tunataka ajitokeze hadharani aseme nini kilimvutia kukataa uteuzi kuwa DC na kuamua kuendelea kuongoza Walumu jambo la pili awaambie Walimu analipwa shilingi ngapi ambazo zimemfanya akatae kazi aliyopewa na Mh Rais"
Aidha amesema mambo mengine wanayohoji ni pamoja na kutokufuata hatua za manunuzi ya tisheti kwa ajili ya Walimu kwenye sherehe za Mei mosi, uhamisho wa Walimu usiokuwa wa utaratibu pamoja na kugawa vyeo bila Kamati tendaji kuhusishwa ipasavyo, kutetea uovu wa baadhi ya Watendaji na kuendelea kusababisha mpasuko ndani ya Chama.