Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vinara 30 wa ujangili tembo wadhibitiwa

43476 Pic+vinara Vinara 30 wa ujangili tembo wadhibitiwa

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mamkala ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini (Tawa) kwa kushirikiana na kikosi kazi za taifa cha kupambana na ujangili, wamefanikiwa kudhibiti mtandao wa majangili baada ya kukamata vinara wa ujangili zaidi ya 30 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi, Naibu Kamishna Tawa ambaye anahusika na uhifadhi na masuala ya ujangili, Mabula Misungwi alisema, kudhibitiwa majangili kumesababisha wanyama hasa tembo kuwa salama nchini.

Alisema hata hivyo, kesi za watuhumiwa hao, baadhi tayari zimefikishwa mahakamani na nyingine zipo katika uchunguzi katika hatua mbalimbali na lengo ni kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa mahakamani. “Tumebaini mitandao ya ujangili kila mmoja unaweza kuwa na watu wanane kuna mnunuzi mkubwa, wanaosambaza fedha, walenga shabaha, kuna wasafirishaji na watoa wa huduma nyingine,” alisema

Misungwi alisema, katika kupambana na ujangili, waliamua kupambana na makundi hayo na wamefanikiwa na sasa Tanzania imekuwa nchi ya mfano barani Afrika kudhibiti ujangili.

“Tulifanikiwa kutokana na kuimarisha intelijensia hasa tunapokamata mtu akiwa na meno ya tembo na aliyehusika kupiga tembo,” alisema.

Alisema kwa sasa hali ni shwari katika mapori ya akiba, mapori tengefu, maeneo ya nje ya hifadhi za taifa na hakuna matukio ya ujangili.

Kamishna Mkuu Tawa, Dk James Wakibara alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa, katika maeneo yaliyokuwa na ujangili kama pori la akiba la Selous hakuna mizigo ambayo inaokotwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz