Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vimelea vya kipindupindu vyabainika kwenye visima Shinyanga

Kenya Yatoa Tahadhari Ya Mlipuko Wa Kipindupindu Vimelea vya kipindupindu vyabainika kwenye visima Shinyanga

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Visima 27 vya maji kati ya 34 vilivyopimwa katika wilaya za Kahama na Kishapu mkoani Shinyanga vimebainika kuwa na vimelea vya Ugonjwa wa Kipindupindu.

Hayo yamebainishwa leo Januari 16, 2024 mjini Shinyanga na Meneja wa Ubora wa Maabara ya Maji Mkoa wa Shinyanga, Marco Kayanda akisema kati ya visima 34 vilivyopimwa, 22 vilikuwa vya Manispaa ya Kahama ambako sampuli 18 zimekutwa na vimelea vya ugonjwa huo.

Amesema visiwa vingine 12 vilivyopimwa vilikuwa vya Wilaya ya Kishapu kati ya hivyo, tisa vimebainika kuwa na vimelea vya Ugonjwa wa Kipindupindu.

Kayanda amesema hatua kadhaa tayari zimechukuliwa ikiwamo kunyunyiza dawa ya kuua vimelea katika visima vyote na kuhakikisha maji yake yanakuwa salama.

Amesema wamejipanga kuendelea kuchukua sampuli maeneo mengine ambayo hawajayafikia na kuweka dawa kwenye visima, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kupata majisafi na salama.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Shinyanga (Ruwasa), Julieth Payovela amesema katika eneo la Mji wa Kagongwa, visima vingi vimejengwa jirani na vyoo, mvua zinaponyesha uchafu unaingia kwenye visima.

Amesema wananchi wengi wanachimba visima bila kufuata utaratibu unaoelekeza visima vijengwe ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyoo, lakini Kagongwa vingi vimejengwa ndani ya mita kumi kutoka vyoo vilipo.

Amesema Kagongwa kuna maji ya Ziwa Victoria lakini wananchi wengi hawatumii, badala yake wanatumia ya visima na kuwaomba wabadilike, watumie majisafi na salama kwa kuwa Ugonjwa wa Kipindupindu ni mbaya na unaua.

Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mulyutu amesema idadi ya wagonjwa wa kuhara na kutapika imefikia 57 na waliothibitika kuwa na kipindupindu ni 18.

Ugonjwa wa Kipindupindu katika Mkoa wa Shinyanga ulithibitika kuingia Desemba 28, 2023 katika Mji wa Kagongwa baada ya wananchi kuanza kuhara na kutapika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live