Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vilio, simanzi vyatawala nyumbani kwa RAS Kilimanjaro

Vilio Nyumbani RAS Mjane wa marehemu Tixon Nzunda, akiwa ameshikiliwa na baadhi ya ndugu wakati

Thu, 20 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Vilio na simanzi vimetawala nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda (56) aliyefariki kwa ajali ya gari yeye na dereva wake wakati mwili huo ulipowasili nyumbani kwake Shanty Town, Manispaa ya Moshi, mkoani humo, saa 10:50, ukitokea Hospitali ya KCMC ulikokuwa umehifadhiwa.

Tixon yeye na dereva wake, Alphonce Edson (54) walifariki juzi Juni 18, 2024 kwa ajali ya gari iliyotokea saa 8:30 mchana katika eneo la Njia panda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye alikuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.

Vijana wa Msalaba mwekundu (Red cross) pamoja na vijana wa Skauti wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda ambaye alifariki kwa ajali Juni 18.

Viongozi mbalimbali wa chama na serikali, viongozi wa dini, watumishi wa serikali mkoani humo, wabunge, wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali pamoja na wananchi wamefika nyumbani hapo kushiriki ibada fupi ya kuaga mwili huo.

Hata hivyo, baada ya mwili huo kuwasili nyumbani hapo umeingizwa ndani kwa ajili ya ibada fupi ya kifamilia na kisha mwili huo itatolewa nje kwa ajili ya ibada maalumu na wananchi waliofika kupata fursa ya kuaga na kutoa heshima za mwisho.

Ratiba iliyotolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema mwili wa Tixon baada ya kuagwa nyumbani kwake leo saa 10 alasiri mwili huo utapelekwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na kisha kusafirishwa kupelekwa Goba, Dar es salaam kwa ndege ya Serikali.

Kesho Ijumaa, Juni 21 mwili huo utapelekwa Songwe kwa mazishi ambayo yatafanyika siku ya Jumamosi, Juni 22.

Chanzo: Mwananchi