Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vilio Dar, Machame

55293 Vlio+pic

Fri, 3 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Moshi. Vilio, majonzi, huzuni vimeikumba nchi kutokana na kifo cha mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi.

Mengi atakayekumbukwa kwa mchango wake katika kila sekta nchini, alifariki dunia usiku wa kuamkia jana akiwa Dubai, Falme za Kiarabu.

Baada ya kutangazwa kwa kifo chake watu wa kada mbalimbali walituma salamu za rambirambi akiwamo Rais John Magufuli na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, wakielezea mchango wa mfanyabiashara huyo maarufu katika ustawi wa nchi.

Hata hivyo, hadi jana saa 1:30 usiku, hakuna taarifa rasmi kuhusu kifo cha mmiliki huyo wa vyombo vya habari vya ITV/Radio One na The Guardian Limited zilizokuwa zimetolewa na familia.

Waandishi wa habari na watu wa kada mbalimbali walianza kumiminika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo kuanzia saa tatu asubuhi jana na kushuhudia mafundi wakirekebisha maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za kifo hicho na utaratibu, msaidizi wa Mengi, Abdulhamid Njovu alisema kutokana na kifo hicho kuwa za ghafla, taarifa kamili zitatolewa na wanafamilia baada ya kuwasiliana na ndugu walioko Dubai.

Ilipofika saa 7:40 mchana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alizungumza na wanahabari kwa niaba ya familia lakini pia alisema kutokana na Mengi kufariki ghafla, ndugu walikuwa wakikutana kuweka mambo sawa kabla ya kutoa taarifa kamili.

Alisema kutokana na ufinyu wa eneo na msiba ulivyowagusa watu wengi, wanafamilia wanaendelea kutafakari eneo litakalofaa zaidi kwa ibada.

Baadaye saa 10 jioni, mwanasheria wa familia, Michael Ngalu alisema maandalizi ya msiba huo yalikuwa yakiendelea na kwamba taarifa za msiba zingetolewa leo mchana.

Watu waliofika nyumbani kwa marehemuwalikaa muda kwa mfupi na kisha kuondoka.

Miongoni mwa watu walifika alikuwa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Hali ilivyokuwa Machame

Kijijini kwake, Nkuu Machame, mkoani Kilimanjaro, ndugu, jamaa, majirani na marafiki wa karibu walifika nyumbani kwa marehemu wakitaka kujua kilichomsibu na utaratibu wa mazishi lakini pia, walielezwa kuwa taarifa ingetolewa baada ya kikao cha familia Dar es Salaam.

Baadhi waombolezaji waliokuwa nyumbani hapo walisema kifo cha Mengi ni pigo kubwa kwa watu wa Machame na Taifa kwa ujumla kwani alikuwa mtu wa watu na alibeba matatizo ya jamii kama yake na kuyafanyia kazi.

Mmoja wa majirani, Grace Nkya alisema watamkumbuka Mengi kwa mchango wake mkubwa katika jamii kwani akisema alikuwa msaada mkubwa katika eneo zima la Machame Nkuu.

“Alikuwa na roho nzuri sana, siku akija Machame watu wanajazana nyumbani kwake na alikuwa habagui mtu yoyote, yaani watu wanajisikia baba kaja nyumbani na ni kutokana na upendo mkubwa aliokuwa nao kwa watu,” alisema Nkya. “Mengi ni mtu ambaye alikuwa akisikiliza watu, yaani ukikaa naye ukiwa mnyonge anakuita taratibu mnaongea wote na sehemu ya kukusaidia anakusaidia.”

Jirani huyo aliungwa mkono jirani mwenzake, Ndeni Nkya aliyesema wamepoteza jirani mwema ambaye alikuwa na upendo wa pekee kwa watu na kusaidia wasiojiweza.



Chanzo: mwananchi.co.tz