Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vikundi Kasulu vyakopeshwa Sh milioni 140                                                                  

5cc17b2f10e7b19b52cce1c9920ed13a Vikundi Kasulu vyakopeshwa Sh milioni 140                       

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VIKUNDI 31 vya wanawake na vijana katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma vimepata mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 140 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Akitoa taarifa ya kutolewa kwa mikopo hiyo Ofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Victoria Makyao alisema kuwa kutolewa kwa mikopo hiyo ni utekelezaji wa takwa la kisheria kwa kila halmashauri nchini kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha wa 2018 hadi Februari mwaka huu, halmashauri ya wilaya ya Kasulu imekwisha toa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni mia nne na laki nane kwa makundi hayo ikiwa ni asilimia kumi ya mapato ya ndani yaliyokusanywa katika kipindi hicho.

Sanjari na mikopo hiyo halmashauri pia imefanikiwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali, utunzaji wa kumbukumbu na elimu ya malezi chanya kwa washiriki wa vikundi hivyo kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuhakikisha vikundi hivyo vinakuwa endelevu.

Akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 140 iliyotolewa kwa vikundi hivyo, mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange alikabidhi pia pikipiki kwa kikundi cha kina mama wa kijiji cha Kigadye kilichopo katika halmashauri hiyo iliyonunuliwa kutoka sehemu ya mikopo hiyo.

Akizungumza Kanali Anange amewataka wanawake wilayani Kasulu kuyatumia maadhimisho hayo kukaa pamoja na watoto na kuwapa maarifa ya mabadiliko yanayotokea katika miili yao hali itakayowawezesha kujitambua na kuepukana na vishawishi.

Akiahirisha sherehe hizo makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Laurent Poteza, amewashauri wanawake kuitumia mikopo wanayoipata kwa malengo yaliyokusudiwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz