Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijiji vinne vyavuna Sh280 milioni hewa ya ukaa Iringa

Hewa Pix Data Vijiji vinne vyavuna Sh280 milioni hewa ya ukaa Iringa

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Vijiji vinne kutoka Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa vimekabidhiwa hundi ya Sh280 milioni baada ya kuwekeza kwenye hewa ya ukaa.

Vijiji hivyo vimevuna mamilioni hayo kutokana na biashara ya hewa ya ukaa wakati dunia ikishuhudia kuendelea kuongezeka kwa joto linaloweza kusababisha madhara ikiwamo ukame na uhaba wa chakula.

Vijiji vilivyonufaika ni Uchindile Sh140 milioni, Mapanda Sh67.4 milioni, Chogo Sh64.4 milioni na Kitete Sh8.4 milioni.

Akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji kwenye Sekta ya Misitu Mkoani Iringa, Meneja wa Mazingira, Jamii na Utawala kutoka Taasisi ya Green Resources, Demetrius Kweka amesema vijiji vilivyonufaika ni vile vilivyotoa ardhi yake kwa ajili ya kuruhusu uvunaji wa hewa ya ukaa.

Amesema moja ya masharti ya kuingia kwenye biashara ya hewa ya ukaa ni kupanda miti kwenye eneo ambalo miaka kumi mfululizo lilikuwa wazi.

“Shamba la miti lililopandwa linatakiwa kuwa limetunzwa kwa zaidi ya mika kumi. Anayechafua mazingira anaweza kununua kibali cha uchafuzi wa mazingira ili kuwalipa wanaopunguza hewa ya ukaa,” amesema Kweka.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mapanda, Obedi Madembo amesema japo wamekuwa wakivuna mamilioni kwa sababu ya hewa ya ukaa bado wanahitaji elimu zaidi kujua suala hilo.

“Tunashukuru kwa fedha hii itakayosaidia maendeleo ya kijiji, ombi letu ni elimu zaidi kwa sababu tukirudi na hii cheki tunaulizwa hewa ya ukaa nini, tunajiuma uma kuelezea. Tunaomba tuendelee kuelimishwa ili tujikite zaidi kwenye hiyo,” amesema

Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi amesema “Naamini tunaweza kunufaika zaidi, na kunahitajika uwazi katika suala hili, mfano ni hesabu zipi zinatumika kuwa kijiji A kinastahili kiasi kadhaa na B kiasi kadhaa,” amesema Chumi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amesema kimeanzishwa kitengo kwa ajili ya kushughulikia masuala ya hewa ya ukaa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA).

Amesema suala la utunzaji wa mazingira ni muhimu na kwamba, kimeanzishwa kitengo kwa ajili ya kushughulikia biashara ya hewa ya ukaa.

Chanzo: mwananchidigital