Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijiji vinne vimepata umeme wa Rea Tunduru

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wakati utekelezaji wa awamu ya tatu ya Mradi wa Umeme Vijijini (Rea), ukiendelea vijiji vinne pekee wilayani Tunduru vimeunganishwa na nishati hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imesema inapanga kuviunganisha vijijini vingine vinne katika mzunguko wa kwanza wa awamu hiyo na vijiji 57 vinavyobaki vitapaswa kusubiri mpaka mwakani.

Taarifa hizo zimebainishwa leo, Mei 8, 2019 na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate aliyetaka kujua ni lini wananchi wa wilaya hiyo watapata umeme.

“Jimbo la Tunduru Kusini lina vijiji 65, tumeshapeleka umeme vijiji vya Azimio, Chiwana, Mkandu na Mbesa. Katika Rea III, vijiji vingine vinne vitaunganishwa navyo ni Mchuluka, Umoja, Namasalau na Msinji (ambavyo) vitaunganishwa katika mzunguko wa kwanza unaotarajiwa kukamilika Juni 2020,” amesema Mgalu.

Baada ya hapo, Mgalu amesema vijiji 57 vinavyobaki vya kata za Chiwana, Mchuluka, Mtina, Nalasi, Mchoteka, Ligoma, Tuwemacho na Lukumbulu vitapata umeme kwenye mzunguko wa pili wa awamu ya tatu ya Rea itakayoanza kutekelezwa Julai 2020 na kukamilika Juni 2021.

Kwenye swali lake, Mpakate amesema jimbo lake lenye vijiji 65 limeachwa nyuma na ni vijiji vinne pekee vimeunganishwa na umeme wa Rea katika awamu mbili zilizopita (Rea I na II) na kuitaka Serikali kueleza ni lini vijiji 61 vilivyobaki vitapata nishati hiyo.

Mgalu amesema kuwa usambazaji wa umeme jimboni humo unahusisha ujenzi wa njia za umeme na ufungaji wa transfoma ili kuwaunganisha wateja wa awali 275 kwa gharama ya Sh644 milioni.



Chanzo: mwananchi.co.tz