Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijiji 60 Nkasi kunufaika na mradi wa LTIP

Nkasi Miliki Ardhi (600 X 277) Vijiji 60 Nkasi kunufaika na mradi wa LTIP

Tue, 9 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) imeendelea kuhakikisha inaongeza thamani katika ardhi za Watanzania ambapo katika Wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa takribani vijiji 60 vitanufaika na mradi huo kwa kupangiwa matumizi ya ardhi ambapo mpaka sasa vijiji 45 matumizi yake yamekwishaandaliwa.

Akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Lazaro Komba alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika ukumbi wa Ngunga, tarehe 08 Aprili 2024 Mkoani Rukwa.

Alisema mbali na mradi wa LTIP kupanga matumizi ya ardhi ya vijiji wilayani humo, mradi umefanikiwa kuhamasisha wananchi takribani 23,220 kuhusu ushiriki wao katika zoezi la uandaaji wa matumizi ya ardhi, jumla ya vyeti vya vijiji 30 tayari vimeandaliwa na vingine 15 viko katika hatua za mwisho ambapo uandaaji wa vyeti hivi utatoa hadhi kwa Halmashauri ya Kijiji kuwa na Mamlaka ya kusimamia Ardhi ya Kijiji husika kwa mujibu wa Sheria.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi huo wilayani Nkasi kwa kuwa utayarishaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji umetoa fursa ya kipekee ya kumaliza changamoto zinazohusiana na matumizi ya Ardhi kama vile migogoro ya mipaka, migongano ya matumizi ya ardhi, uharibifu wa mazingira na ukosefu wa Usalama wa Milki za Ardhi kwa wananchi.

‘‘Ongezeko la idadi ya watu limeongeza kasi ya ukuaji wa vijiji vyetu na baadhi ya vitovu vya vijiji kubadilika kuwa vijiji miji hasa Chala, Kirando, Kabwe Asilia, Kipili na maeneo mengine hivyo uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na wananchi kutapunguza au kumaliza kabisa kwa migogoro ya ardhi, kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii na utunzaji wa mazingira’’ alisema Komba.

Aidha aliwataka Waheshimiwa Madiwani wote, Watendaji wa Kata na Vijiji kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha utekelezaji wa Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live