Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana waoywa kudai urithi kabla ya vifo vya wazazi

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbulu. Vijana wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, wametakiwa kutoanzisha migogoro ya kifamilia ikiwemo kudai urithi kabla wazazi wao hawajafariki dunia. 

Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga aliyasema hayo jana Jumapili Novemba 25, 2018 wakati akizungumza na wananchi waliofika ofisini kwake kutatuliwa migogoro yao. 

Mofuga alisema mtindo wa baadhi ya vijana wa Mbulu kutaka kuandikiwa mirathi ilhali wazazi wao hawajafa si jambo zuri kwani ni tofauti na mila na desturi za Kitanzania. 

"Vijana fanyeni kazi bado mna nguvu za kutosha, zitumieni kwa kujiwezesha kiuchumi kuliko kutaka kupewa urithi kabla ya wazazi wenu hawajatangulia mbele ya haki," alisema Mofuga. 

Alitoa onyo kwa vijana watakaokuwa wanashinikiza wapewe urithi kabla ya wazazi kufariki dunia kwani atawachukulia hatua kali ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia hiyo. 

"Kesi za namna hiyo zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku, sasa nataka ifike mwisho vijana badilikeni kwa kufanya kazi za kuzalisha mali ikiwemo kilimo na si kutaka urithi kabla wazazi hawajafariki dunia," alisema Mofuga. 

Pia alikemea vikali mila potofu za kutenga watu na baadaye kuvamia mali na kupora mifugo inayofanywa na baadhi ya viongozi wa mila kwenye eneo hilo. 

Baadhi ya wakazi wa Mbulu, wamepongeza hatua ya mkuu wa mkoa kwa madai kuwa vijana wengi wamekuwa wanashinikiza wapewe urithi kabla ya wazazi kufariki dunia. 

Mkazi wa eneo la Ayamohe, Anthony Bura alisema kitendo cha kudai urithi kwa wazazi kabla hawajafariki dunia si sahihi kwani ni uchuro kwa jamii inayowazunguka. 

Bura alisema ni vyema vijana hao wakajikita kwenye shughuli za maendeleo kuliko kung'ang'ania kupewa urithi ilhali bado wana nguvu za kujitegemea. 

Lucy Jacob alisema ana uhakika baada ya kauli hiyo ya mkuu wa wilaya kuwafikia vijana, watabadilika na kuachana na mtindo huo wa kutaka kuandikiwa mirathi kabla ya wazazi wao kufariki dunia. 

"Wanapaswa kutambua kuwa kazi ndiyo msingi wa maendeleo na wengine wamesomeshwa na wazazi lakini wanashindwa kuitumia elimu hiyo iwasaidie badala yake wanataka urithi kabla ya wakati," alisema Jacob. 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz