Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana wachangamkia fursa ya ufugaji nyuki

77785 Pic+nyuki

Mon, 30 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ufugaji wa nyuki umeanza kuwa kivutio kwa Watanzania wengi hasa vijana baada ya kuelezwa kuna soko kubwa la asali na nje ya nchi hiyo.

Hilo limeonekana kwenye maonyesho ya bidhaa za utamaduni ya Tamasha la Utamaduni la Afrika Mashariki (Jamafest) yaliyomalizika jana Jumamosi Septemba 28, 2019 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Idadi  kubwa ya vijana kwenye banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakipewa elimu kuhusu ufugaji nyuki kisasa unaochochea mavuno makubwa ya asali.

Ofisa anayehusika na ufugaji wa nyuki wa TFS, Juma Mdoe alisema kumekuwa na mwamko mkubwa wa watu kutaka kufahamu kuhusu ufugaji wa nyuki na ndiyo sababu walitumia Jamafest kama fursa ya kutoa elimu kwa umma.

Alisema  mazao yatokanayo na ufugaji nyuki yamekuwa yakiingiza kipato kikubwa kwa wafugaji na kwa taifa kwa ujumla hivyo ni fursa inayopaswa kuchangamkiwa.

“Ufugaji wa nyuki ni fursa, inaonekana watu wameanza kuichangamkia kama hivi wanakuja kujifunza na wanauliza maswali hii inaonyesha wana kiu ya kutaka kujua kwa kina,” alisema

Pia Soma

Advertisement
“Tunachoendelea kuwasisitiza vijana na watu wanaoendelea kujifikiria, ufugaji wa nyuki unalipa na soko lipo ndani na nje ya nchi. Tuwe tayari kufuga kisasa,” aliongeza

Akizungumza akiwa katika banda hilo, Ramadhan Kihailo ambaye ni mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam alisema amekuwa na shauku ya kuingia kwenye ufugaji huo lakini alikuwa hana uelewa wa kutosha.

“Huwa nasikia kuhusu ufugaji wa nyuki na faida zake na ninatamani sana kwa sababu mimi ni mtumiaji mzuri wa asali. Changamoto niliyokuwa nayo sijui naanzia wapi ndiyo maana nilipofika hapa na kukuta wataalam nikataka kujifunza,” alisema

Katika hatua nyingine ofisa misitu John  Selestine alisema TFS imetumia Tamasha la Jamafest kutangaza misitu ya hifadhi ya mazingira asilia  iliyopo nchini na vivutio ambavyo havipatikani sehemu nyingine duniani.

“Uwepo wa viumbe na mimea ambavyo havipatikani kokote ndio imesababisha tuwe na urithi na kufanya misitu hiyo ya pekee. Tunawaalika watu kutoka sehemu mbalimbali kutembelea misitu yetu,” amesema Selestine

Chanzo: mwananchi.co.tz