Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana 400 masikini wafadhiliwa masomo-ANCHOR

44f0918db24ca496d539c65f8dfa5e2b Vijana 400 masikini wafadhiliwa masomo-ANCHOR

Wed, 13 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

ZAIDI ya vijana 400 kutoka familia masikini wamepata ufadhili wa masomo ya fani mbalimbali za afya katika Chuo cha Afya cha Tandabui (TIHEST) kilichopo jijini Mwanza.

Wanafunzi hao wawezeshwa kusoma chuoni hapo kati ya mwaka 2012 na 2020 ikiwa ni sehemu ya mpango maalumu wa chuo hicho unaolenga kutoa elimu ya juu bure kwa watoto kutoka familia maskini.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo cha Tandabui, Dk Wallace Keto alisema wanafanya hivyo ili kutoa mchango wao kwa jamii, lengo likiwa ni kumsaidia Rais John Magufuli kutimiza ndoto zake za kuwasaidia Watanzania wanyonge hasa katika sekta ya afya.

“Afya bure ni jambo muhimu katika maendeleo, nchi yetu haiwezi kuendelea bila kuwa na watu wenye afya nzuri. Afya bora ni nguzo muhimu katika maendeleo ya viwanda na sekta nyingine,” alisema.

Mkuu huyo wa chuo alisema ili kufanikisha dhamira ya Rais Magufuli ya kuwasaidia wanyonge na kutimiza ndoto ya uchumi wa viwanda, lazima kuwe na wataalamu wa afya wa kutosha wanaoweza kutoa huduma bora kwa Watanzania mpaka katika ngazi za vijiji.

Kwa mujibu wa Dk Keto, mpango wa kuwasaidia wanafunzi wasio na uwezo umeanza miaka minane iliyopita chuo kilipo anzishwa na kwamba mwaka huu wa taaluma wanatarajia kutoa ufadhili kwa wanafunzi 100 kutoka familia maskini kusoma kozi mbalimbali za afya chuoni hapo.

Akizungumza baada ya kuwatunuku vyeti wanafunzi 1,935 wa Chuo cha Tandabui wakati wa mahafali, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Phiris Nyimbi alisema wafaidika wa ufadhili wa nafasi 100 watosoma kozi za uuguzi, famasia, utabibu, maabara, utunzaji kumbukumbu za afya na afya ya jamii.

Aliahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazokwamisha juhudi za utoaji elimu chuoni hapo na kutoa rai kwa wahitimu kutumia ujuzi na taaluma waliyopata kusaidia Watanzania kupata elimu bora ili kuliwezesha taifa kupiga hatua za maendeleo.

Chanzo: habarileo.co.tz