Takriban vijana 400 kutoka Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, wanatarajia kupewa mafunzo ya ujuzi na maarifa muhimu kwa ajili ya maendeleo binafsi.
Hilo linatarajiwa kufanyika wilayani humo na kampuni ya Serengeti Breweries Limited kupitia programu yake ya 'Learning for Life'.
Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema hatua hiyo itachagiza ukuaji wa maendeleo ya wilaya hiyo.
"Hatua hii ni muhimu kwa mkoa wetu na inakwenda sambamba kikamilifu na lengo la Wilaya ya Hanang la kutoa huduma bora na zilzio endelevu ifikapo mwaka 2025," amesema.
Kulingana na Sendiga, hatua hiyo itaunda kundi la watu wenye ujuzi na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya na uvumbuzi katika jamii.
Meneja wa Mawasiliano wa Serengeti Breweries Limited, Rispa Hatibu amesema mafunzo hayo yameanza leo na yatakamilika Septemba 21, mwaka huu.
"Tunaamini kuwekeza kwa vijana ni kulinda mustakabali wa jamii yetu. Kupitia programu ya Kujifunza kwa Maisha, tunatoa ujuzi pia inakuza uwezo wa vijana wa Hanang kuwa viongozi, wajasiriamali, na wachangiaji katika ukuaji na mafanikio ya wilaya hii," amesema.