Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana 30 wakopeshwa milioni 20/-

792b43f9db294be6e8593acd3efe29bb Vijana 30 wakopeshwa milioni 20/-

Mon, 8 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya Mji wa Babati Mkoa wa Manyara imeendelea kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imetoa mkopo wa Sh milioni 20 kwa vikundi vya vijana 30 katika Kata ya Bagara.

Hayo yamesemwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Amina Masood wakati akisoma taarifa ya utoaji mikopo kwa vikundi katika kata ya Bagara kwa uongozi wa UWT na CCM uliotembelea vikundi vya ujasiriamali, Aliwataka walengwa kuchangamkia fursa ya kujipatia mikopo hiyo isiyo na riba kutoka serikalini ili kufanya shughuli za kujikwamua na umasikini.

Alisema mikopo hiyo itaviwezesha vikundi kupanua mitaji yao na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora utakaokubalika na Shirika la Viwango nchini (TBS).

“Bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya soko na kuongeza fursa za ajira kwa vijana, akina mama na kukuza mapato ya Halmashauri,” alisema.

Alibainisha kuwa baadhi ya vikundi vimekuwa havirejeshi mkopo kwa wakati ili vikundi vingine viweze kukopa kwa wakati, jambo linalorudisha nyuma jitihada za halmashauri hiyo.

Alisema kuwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2015/2016 mpaka 2019/2020, halmashauri hiyo katika Kata ya Bagara, ilitoa mikopo ya Sh 236,943,891.15 na wanufaika ni 490, wanawake ni 359, vijana 125 na watu wenye ulemavu sita.

Akizungumzia mikakati mbalimbali iliyowekwa na halmashuari ili kuhakikisha wanawake, vijana na walemavu wa Babati wanaunda vikundi na kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo hiyo, Amina alisema kuwa serikali kupitia idara hiyo imesogeza ofisa maendeleo ya Jamii kila kata ili wananchi wapate elimu juu ya uundaji wa vikundi na kupata mikopo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Babati, Elizabeth Malle aliishauri halmashauri hiyo kuendelea kutoa elimu ya kujua utaratibu wa kupata mikopo na kujizatiti kuongeza vyanzo vya mapato katika halmashauri na kuzuia mianya ya wanaokwepa kulipa kodi zinazotozwa na halmashauri.

Ujumbe huo wa CCM ulitembelea kikundi cha ufugaji wa kuku na bucha ya nyama ya kuku, Kikundi cha Kibatima kilichopo Mtaa wa Nyunguu kinachojishughulisha na uuzaji wa batiki ili kujionea jinsi walivyotumia mikopo hiyo ya serikali kujianzishia miradi ya maendeleo na kujiingizia kipato.

Pia walitembelea kikundi cha vijana kinachotengeneza vifungashio cha Mind Plus Capital na kikundi cha wanawake cha ufugaji Kuku cha Sayari.

Mwenyekiti wa kikundi cha Kuku Investment, Salimu Saguma na Katibu wake, Sabinate Karunde alisema kuwa mkopo umewasaidia kupata marejesho ya kila mwezi na kuweza kukopeshana wao kwa wao.

Mwenyekiti wa kikundi cha Mind Plus Capital, Clinton Joseph aliitaka serikali kuwatafutia soko la mifuko na vifungashio vinavyotengenezwa kwa karatasi, kwani kikundi chao kina uwezo wa kutengeneza mifuko 1,000 hadi 3,000 kwa siku.

Chanzo: habarileo.co.tz