Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limewatia mbaroni watu saba wakituhumiwa kuiba mifuko 390 ya saruji, mali ya mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Wilbroad Mtafungwa alisema tukio hilo lilitokea Machi 8 mwaka huu saa 3.00 usiku katika Kijiji cha Bushini wilayani Kwimba. Kamanda Mtafungwa alisema siku hiyo polisi walimkamata Masele Shija (35), mkazi wa Misungwi akiwa na mifuko 390 ya saruji aina ya twiga, mali ya mradi wa SGR.
Alisema saruji hiyo ni sehemu ya mifuko 600 aliyokabidhiwa dereva wa kampuni ya TEXAS Juma Michael (29) kwa ajili ya kuisafirisha kwenda kwenye ghala la SGR lililoko Nyashishi. Kamanda Mtafungwa alisema mifuko hiyo ilikamatwa ikiwa kwenye nyumba ya Shija na kwamba awali ilikuwa imehifadhiwa kwenye ghala kwa ajili ya kupelekwa kwenye mradi wa SGR katika eneo la Bukwimba.
Aliwataja wengine waliokamatwa na wanaohusishwa kwenye tukio hilo ni raia wa China mtunza stoo na mkazi wa Bukwimba, Meng Zion (29). Alisema raia huyo wa China amekamatwa kwa sababu kumbukumbu za utunzaji wa stoo na usafirishaji wa mizigo zinaonesha mifuko 600 ya saruji ilipokelewa hapa stoo.