Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vibanda vya biashara vyateketea, gari la Zimamoto likisubiri ndege kuruka

90373 MOTO+PIC Vibanda vya biashara vyateketea, gari la Zimamoto likisubiri ndege kuruka

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Uchache wa vitendea kazi umechangia kikosi cha zimamoto kushindwa kuzuia vibanda 25 vya biasharra katika soko la Sabasaba kuteketea baada ya magari yake mawili kuwa katika matukio tofauti wakati moto ulipoanza.

Kwa mujibu wa mashuhuda, moto huo ulianza saa 12:45 jana asubuhi lakini juhudi zao za kuita gari la zimamoto hazikufanikiwa kwa kuwa moja ya magari mawili yaliyopo mkoani hapa lilikuwa likisubiri ndege kupaa na jingine lilikuwa limekwama, Mwananchi imeelezwa.

Walisema moto huo umeteketeza zaidi ya vibanda 25 kati ya vibanda zaidi ya 120 vilivyopo eneo hilo la soko.

Vibanda hivyo vya wafanyabiashara wadogo ambavyo vimeungua ni pamoja na vya mama lishe, saluni za kike na kiume, maduka ya simu, maduka ya nguo za mitumba na mpya na vibanda vya vocha na vya huduma za miamala ya simu.

Mmoja wa wafanyabishara anayeuza simu eneo hilo, Adam Makumburu aliiambia Mwananchi kuwa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji lilichelewa kufika na hivyo vibanda kuendelea kuteketea.

Alisema bidhaa zilizokuwa ndani ya kibanda chake za thamani Sh25 milioni zimeteketea zote. Kwa upande wake mwenyeti wa soko hilo, Edward Ndahani alisema wanaendelea na tathmini ya mali iliyoteketea.

“Lakini kwa kifupi ni kuwa vilivyoungua ni vya saluni, mama lishe, vya kuuzia simu na vifaa vingine vya simu, nguo za mitumba na za dukani,” alisema Ndahani.

Akizungumzia tukio hilo, kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Dodoma, Gilbert Mvungi alisema walipata taarifa za tukio hilo saa 12:48 asubuhi, lakini walishindwa kufika kwa wakati kwa sababu gari lilikuwa uwanjani kwa ajili ya ndege iliyokuwa inaruka muda huo.

“Taarifa tulizipata mapema lakini kulikuwa na uchelewaji kwa sababu tulikuwa uwanja wa ndege na tuliondoka saa 1:33 asubuhi baada ya ndege kupaa ili kuelekea eneo la tukio na hii imesababishwa na kukwama kwa gari moja katika eneo la Kisasa Mwangaza kwa sababu ya mvua zinazoendelea kunyesha,” alisema kamanda Mvungi.

“Tuna gari mbili moja tunalitumia upande wa mji na jingine kwa shughuli za uwanja wa ndege. Jana tulipata tukio maeneo ya Kisasa Mwangaza na yaliondoka magari yote mawili, lakini kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha gari inayotumika kwenye shughuli za uwanja wa ndege lilikwama na mpaka sasa juhudi za kuitoa zinaendelea. “Gari iliyobaki ilibidi tuipeleke uwanja wa ndege maana kuna ndege iliyokuwa inapaa hivyo tukachelewa kufika kuokoa mali zilizokuwa zinateketea,” alifafanua kamanda huyo.

Zilipo ofisi za jeshi hilo hadi kufika eneo la tukio ni umbali wa kutumia dakika moja kwa usafiri wa gari, na pia umbali wa kutoka uwanja wa ndege hadi eneo hilo ni mwendo wa dakika tano kwa gari sawa na umbali wa kilomita takriban tatu.

Akizungumzia zaidi kuhusu tukio la moto huo, kamanda Mvungo hata hivyo alisema kwamba baada ya kufika walifanikiwa kuzima moto uliotekeza vibanda 26 na kuokoa vingine ili visiungue.

Alisema kwamba changamoto kubwa waliyoipata ni utaratibu mbaya uliotumika kujenga vibanda hivyo, kwa kuwa hakuna nafasi ya kutosha kuruhusu gari kuingia hadi ndani. Kuhusu kushirikishwa katika ujenzi wa vibanda hivyo alisema kwamba watu wa halmashauri ndiyo waliotakiwa kusimamia ujenzi huo na zimamoto kazi yao ni kushirikishwa katika michoro ya majengo ili kutoa ushauri wa kitaalamu kabla ya ujenzi kuanza.

Alisema kutokana na changamoto hiyo leo atakutana na viongozi wa soko hilo ili kujadiliana namna ya kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Pia, alisema kwamba baada ya kukutana na viongozi hao, atakutana na uongozi wa Jiji la Dodoma na baadaye Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kujadiliana namna bora ya kukabiliana na matukio ya aina hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz