Zaidi ya vibanda 3,000 vya wafanyabiashara wadogo, maarufu kama Machinga katika Soko la Ukwaju, vimeteketea kwa moto ambao uliwaka kwa zaidi ya saa tano huku chanzo kikiwa bado kinachunguzwa.
Wakizungumza na Nipashe katika eneo hilo maarufu kama Bango la Zain, baadhi ya mashuhuda na wafanyabiashara wenye vibanda walisema moto huo ulizuka majira ya saa 2:00 asubuhi huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likishindwa kufika kwa wakati kutokana na gari kupata ajali.
Mmoja wa mashuhuda, Bahati Gavani, alisema katika soko hilo kulikuwa banda moja ambalo halitumiki lililokuwa na nyuki na kwamba kulikuwa na viashiria kulikuwa na watu wanarina asali kwa kutumia moto.
“Hao nyuki walikuwapo kwa muda mrefu katika banda hilo lililotengenezwa kwa dari (ceiling board), hivyo wakati soko linaungua, tuliona kama kulikuwa na mtu anavuna asali kwenye banda hilo,” alisema Gavani.
Mfanyabiashara Naomi Shema alisema vibanda hivyo walivijenga kutokana na agizo la serikali kuwataka kutoka maeneo yasiyo rasmi na kuwa waliyajenga kwa mikopo ambayo bado wanailipa.
Kuhusu bidhaa, Shema alisema kwenye vibanda hivyo hawakuwa na bidhaa kutokana na wafanyabiashara hao kurejesha shughuli zao katika maeneo walikoondolewa awali kutokana na kukosa huduma muhimu sokoni hapo.
“Tunaomba serikali itusaidie kurejesha miundombinu ya vibanda vyetu kwani kwa sasa hatuna uwezo kabisa wa kuvijenga tena kwa sababu mikopo yenyewe tulikopa ili kuvijenga bado hatujakamilisha urejeshwaji wake,” alisema Debora Omary.
Mwenyekiti wa Soko hilo, John Paulo alisema soko hilo lilianzishwa Oktoba, 2021 kutokana na maelekezo ya Rais kuwa Machinga wapangwe na kuondolewa katika maeneo yasiyo rasmi na wengi waliitikia agizo hilo.
“Hapo kila banda lilijengwa kwa gharama za wastani wa Sh. 360,000 lakini kutokana na kutokuwapo kwa baadhi ya huduma muhimu na wateja, wafanyabiashara walirejea katika maeneo yao ya awali,” alisema Paulo.
Alisema baada ya kutokea kwa moto huo, walijulishwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao wakati wanakwenda katika tukio hilo, gari lao lilipata ajali kisha kutumwa lingine ambalo lilifika kwa kuchelewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilbroad Mutafungwa, alisema katika tukio hilo hakuna majeruhi wala kifo kwa kuwa hakukuwa na watu katika eneo hilo.
“Tulipopata taarifa hiyo tulifika na kukuta tayari moto ni mkali na kushirikiana na wananchi waliokuwapo kuudhibiti wakati tukawajulisha wenzetu wa zimamoto. Hakuna mtu aliyepoteza maisha wala aliyejeruhiwa na vibanda vichache vya barabarani vilivyokuwa na mali wafanyabiashara walijitahidi kuziondoa,” alisema.
Pia alisema vibanda vingi havikuwa na mali na kuwa walishirikiana na Shirika la Umma Tanzania (TANESCO) ambao waliwahi kukata umeme ili kudhibiti madhara zaidi.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Mutafungwa alisema kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo huku akiwaonya wananchi kutokuingia katika eneo hilo kwa ajili ya usalama wa mali za wafanyabiashara, yakiwamo mabati.