Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viazi, maharage vyaua watoto 3 familia moja

9af02118b1157b10866dc59579ea78be Viazi, maharage vyaua watoto 3 familia moja

Wed, 19 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATOTO watatu wa familia moja wamekufa baada ya kula viazi vitamu na maharage pori vinavyosadikiwa kuwa na sumu.

Watoto wengine watatu wa familia hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga amewataja watoto walioaga dunia kuwa ni Kabula Yohana (6), Modesta Makoye (4) na Ezekiel Yohana (3) ambao walikuwa wakiishi katika kijiji cha Igongwe wilayani Mpanda

Alisema mkasa huo ulitokea Agosti 16, mwaka huu saa 12 jioni katika kijiji cha Igongwe kata ya Stalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya Mpanda mkoa wa Katavi.

"Watoto hao watatu kwa nyakati tofauti walifariki dunia baada ya kula viazi vitamu na mbegu za mmea pori unaofanana na maharagwe vinavyosadikiwa kuwa na sumu,"alisema Kamanda Kuzaga.

Alisema siku ya tukio mchana watoto hao wakiwa na wenzao wengine watatu, Yona Sabuni (4), Christina Yohana (4) na Paulo Yohana (6) walikula vyakula hivyo na kuanza kuumwa tumbo.

"Kwa pamoja walichuma mbegu za mmea pori mfano wa kunde na kula pamoja na viazi vitamu vilivyopikwa na baada ya muda hali zao zilibadilika na kuanza kuhisi maumivu makali ya tumbo wakati huo wazazi wa watoto hao ambao ni Yohana Ellias na Agnes Lucas wao walikuwa shambani na hivyo kukosa msaada," alisema Kamanda Kuzaga.

Alisema, saa 12.30 jioni jirani yao aliyetajwa kwa jina la Amos Antony aliwakuta watoto hao wakiwa wamelala chini wakilalamika maumivu ya tumbo.

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, Antony aliwapeleka watoto hao kwenye kituo cha afya cha Sitalike kwa matibabu na hali zao zilizidi kuwa mbaya.

Alisema, wakati wakiwa kituoni hapo, watoto wawili Kabula na Ezekiel walipoteza maisha na waliobaki walikimbizwa katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.

"Ilipotimu saa tatu usiku, mtoto mwingine aitwae Modesta Makoye naye alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Katavi...watoto wawili Yona Sabuni na Christina Yohana bado wamelazwa Hospitali Teule ya Rufaa Mkoa wa Katavi wakiendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri," alisema Kamanda Kuzaga.

Alisema, baada ya tukio hilo madaktari walifanya uchunguzi wa kitabibu katika miili ya marehemu wote watatu na walikabidhi ripoti kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Kamanda Kuzaga alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo. "Uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini aina ya sumu iliyosababisha vifo kwa watoto hao," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz