Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Wamachinga Mwanza wavamia polisi kushinikiza wenzao kuachiwa huru

Video Archive
Fri, 15 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Ni kama utimilifu wa usemi wa “umoja wetu ndiyo nguvu yetu” imetimia baada ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga zaidi ya 200 wa jijini Mwanza nchini Tanzania kuandamana, kushinikiza na hatimaye kufanikisha kuachiwa huru kwa viongozi wao waliokuwa wakishikiliwa na polisi.

Maandamano ya wafanyabiashara hao wanaofanya shughuli zao katikati ya jiji la Mwanza nchini Tanzania yamefanyika leo Ijumaa Novemba 15, 2019 kwa kundi hilo kuweka kambi kuzunguka Kituo Kidogo cha Polisi cha Pamba kushinikiza viongozi wao walikuwa wakishikiliwa humo kuachiwa huru.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Phillis Nyimbi, Mkurugenzi wa jiji, Kiomoni Kibamba pamoja na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro wamefika eneo la tukio kuwasikiliza wafanyabiashara hao walioweka msimamo wa kutoondoka hadi mwenyekiti wao wa Wilaya ya Nyamagana, Juma Sumuni na Shida Faris waachiwe.

Akitumia mbinu ya kidiplomasia, Kamanda Muliro licha ya kuamuru kuachiwa huru kwa waliokuwa wanashikiliwa, pia amefanikiwa kuwatuliza wafanyabiashara hao kwa kuwataka kutumia njia ya majadiliano na mawasiliano kwa viongozi kutatua changamoto zinazowakabili badala ya maandamano na vurugu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mfanyabiashara Senifa Wambura ameulalamikia uongozi wa jiji kwa kuwahamishia eneo la Miti Mirefu jirani na Hospitali ya Aga Khan alikosema shughuli zao zingeathiri huduma na utulivu kwa wagonjwa.

“Juzi jiji wametupeleka eneo la Mirongo jirani na shule za Thaqaafa, Mirongo, Nyakabungo na Lake. Licha ya kuwa ndogo, uwepo wetu pale pia utaathiri shughuli za masomo kwa wanafunzi na walimu; tunaomba tutafutiwe eneo kubwa na yenye mazingira rafiki,” amesema Wambura

Kutokana na hoja hizo, Mkuu wa wilaya ameagiza kuundwa kwa kamati ndogo itakayoshirikisha Wamachinga, Jiji na wadau wengine kutafuta maeneo yanayofaa wafanyabiashara hao kuhamishiwa kupisha mradi wa ujenzi wa soko kuu mpya katikati ya jiji.

Chanzo: mwananchi.co.tz