Korogwe. Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martin Shigella ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kufanya tathmini ua ujenzi wa daraja la Mandera wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga.
Daraja hilo limevunjika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Tanga na mikoa jirani na kusababisha mito kujaa maji na kuathiri madaraja, huku baadhi ya barabara zikiwa hazipitiki kutokana na maji kujaa.
Shigella ametoa agizo hilo leo Jumamosi Oktoba 26, 2019 baada ya kutembelea daraja hilo lililovunjika na kusababisha magari zaidi ya 300 yaliyokuwa yakitoka mikoa ya Kaskazini na nje ya nchi kuelekea Dar es Salaam kukwama.
Akizungumza na Mwananchi, Shigella amesema baada ya kuruhusu magari kupita, ameagiza Tanroads kufanya tathmini ya uboreshaji wa daraja hilo.
“Nimewataka wafanye tathimini ya ujenzi wa daraja, pia kukarabati sehemu korofi, nimewaomba JWTZ wasaidie na wamekubali,” amesema mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga.
Shigella amewataka madereva kuwa makini na kubainisha kuwa ajali iliyotokea Wilaya ya Handeni na kuua watu ilitokana na dereva kupuuza maelekezo ya polisi.
Pia Soma
- Vikwazo kwa Zimbabwe vyazua mengine mapya
- Wananchi wajitokeza kwa wingi kuipokea Dreamliner Dar
- Mwanajeshi wa Urusi awafyatulia wenzake risasi