Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Wakuu wa shule waliowafukuza wanafunzi kuepuka corona waonywa

VIDEO: Wakuu wa shule waliowafukuza wanafunzi kuepuka corona waonywa

Fri, 20 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo amewaonya wakuu wa shule  wanaowafukuza wanafunzi bila kuwawekea utaratibu wa kusafiri akisema tabia hiyo ni hatari kwa wanafunzi.

Jafo ametoa kauli hiyo leo Machi 20, 2020 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  kufungwa kwa shule kutokana na agizo la Waziri Mkuu ili kuepuka kusambaa kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona.

Waziri Jafo amemtaja Mkuu wa shule ya Sekondari ya Dakawa  mkoani Morogoro kwamba kitendo alichokifanya cha kuwafukuza wanafunzi, ni udharirishaji mkubwa na hatari kwa wanafunzi ambao wengi walionekana kuzagaa na hata kulala stendi za mabasi.

Amesema kuwafukuza wanafunzi shuleni bila kufuata utaratibu, inakuwa hatari zaidi kuliko tatizo lenyewe na akaomba wakuu wa wilaya na wakurugenzi kufuatilia katika shule zote ili uwepo utaratibu mzuri wa kuwasafirisha wanaoishi mbali.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo,  bajeti za vyakula kwa watoto hao zipo na kuwa suala la kuondoka ni lazima waondoke lakini kwa utaratibu mzuri ili watakaokuwa na changamoto waweze kuendelea kuwa shule walau kwa siku chache hadi wawekewe utaratibu mzuri.

“Wakuu wa mikoa wapo Dodoma kushughulikia bajeti zao, lakini kule wamewaacha wakuu wa wilaya na wakurugenzi, nawaagiza wachukue hatua hizo mara moja katika kuhakikisha watoto wetu wanasafiri bila kubughuziwa,” amesema Jafo.

Katika hatua nyingine kiongozi amewamwagia sifa wakuu wa Shule za Sekondari za Kilakala na Dodoma kwamba walifanya vizuri kwa kukubali wanafunzi ambao wanatoka mbali kuendelee kubaki kwa muda wakishughulikia usafiri huku mkuu wa shule ya Dodoma akiwapakia wanafunzi kwa mkopo ili imradi wasafiri salama katika mabasi yanayoaminika.

Chanzo: mwananchi.co.tz