Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Simulizi aliyekaa majini siku 3 baada ya MV Nyerere kuzama

Fri, 20 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Ikiwa ni mwaka moja kamili tangu kivuko cha MV Nyerere kizame kwenye Ziwa Victoria mkoani Mwanza, manusura wa ajali hiyo Augustino Charahani aliyekaa majini siku tatu amesimulia jinsi anavyoikumbuka siku hiyo.

Mbali na kumshukuru Mungu, Charahani anashauri kuwe na kumbukizi maalumu kuwaenzi wanaonusurika katika ajali kama hizo.

Charahani aliyekuwa fundi mkuu wa kivuko hicho, amezungumza na Mwananchi eneo la Luchelele anapoendelea na shughuli hiyo katika kivuko kingine kinachofanya safari kati ya Luchelele wilayani Nyamagana na wilaya ya Sengerema.

Kivuko cha MV Nyerere kilizama Septemba 20, mwaka jana mita chache kabla ya kutia nanga kikitokea Bugorora kwenda Bwisya Ukara wilayani Ukerewe na kusababisha vifo vya watu 231 na wengine 41 kuokolewa.

Marehemu ambao hawakutambuliwa na ndugu zao walizikwa katika makaburi ya pamoja katika viwanja vya Shule ya Msingi Bwisya ambapo pia ulijengwa mnara huku Rais John Magufuli akiagiza kijengwe kituo kikubwa cha afya katika kijiji cha Bwisya.

“Ninapokumbuka tukio hilo, hata sina cha kusema zaidi ya kumshukuru Mungu maana ulikuwa ni muujiza wa pekee, hakuna aliyedhani ningeweza kutoka ndani ya maji nikiwa hai,” alisema. Wakati kivuko kilizama Septemba 20, Charahani aliokolewa Septemba 22 majira ya jioni.

Pia Soma

Advertisement
Charahani anasema kinachomuumiza zaidi wakati akikumbuka siku hiyo ni kuondokewa na mke wake, Cecilia Daniel ambaye angetamani kuwa naye katika kumbukizi hiyo.

“Mke wangu ambaye alikuwa ameshajiandaa kwa ajili ya mazishi yangu wakati huo, kwa sasa tunavyoongea ameshatangulia mbele ya haki hilo ndilo najisikia kuniuma sana,” anasimulia.

Alisema mkewe alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni 30 mwaka huu kwa ugonjwa wa homa ya mapafu baada ya kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Pia manusura huyo anasema jambo jingine linalomfanya akumbuke zaidi ajali hiyo ni mtoto wake ambaye alishindwa kuendelea kidato cha nne na kukariri kidato cha tatu kutokana na kuathirika kisaikolojia kwa sababu ya tukio hilo la baba yake.

“Yule binti yangu alikuwa akilia nani sasa atakayemsomesha shule baada ya mimi kufariki, kwa hiyo hali hiyo ilimvuruga sana hata aliponiona hakuamini, mfumo wake wa shule uliharibika na kulazimika kurudia kidato cha tatu maana hakuweza kufanya mtihani wa kwenda kidato cha nne, lakini nashukuru Mungu kwa sasa anaendelea vizuri na masomo yake kama kawaida,” alisema.

Charahani mwenye watoto wanne, kati yao wawili wa kiume, anasema akiunganisha matukio hayo yote anapata ugumu lakini kikubwa anamshukuru Mungu maana huenda yote yaliyotokea yana sababu zake.

Amshukuru Rais Magufuli

“Namshukuru Rais baada ya kujua kwamba kuna mtu bado yupo hai aliagiza waokoaji kuhakikisha natoka nikiwa hai, na kweli jitihada zilifanyika nawashukuru na viongozi wote waliosimamia kazi hiyo,” anasema.

Charahani anasema “tujaribu kujifunza na ikiwezekana kuwaenzi wanaonusurika kwenye matukio kama haya, japo hatuombei yatokee lakini iwepo kumbukizi maalumu.”

Alisema katika jamii inayomzunguka wapo wanaoona kitu cha kawaida, lakini kiukweli sio jambo la kawaida wapo watu kutoka nje ya nchi wanatamani kumuona. “Nikienda sehemu zingine ikitokea wakajua mimi ndiye nilikaa majini siku tatu huwa ni mshangao mkubwa nakuwa kama kivutio.”

Chanzo: mwananchi.co.tz