Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Risasi ilivyompa ulemavu wa mguu Kayuni

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Wahenga walisema “hujafa hujaumbika” na “hakuna aijuaye kesho yake.”

Semi hizo za wahenga zinasawiri simulizi ya mkazi wa Mtaa wa Ilumbila jijini Mbeya, Lucas Kayuni (52), ambaye ana ulemavu wa mguu wake wa kulia aliopigwa risasi kisha ukakatwa.

Kayuni, mzaliwa wa Kijiji cha Luswisi wilayani Ileje Mkoa wa Songwe, alihamia Ilumbile mwaka 1990 baada ya kuoa. Na alihamia kwa lengo la kutafuta maisha.

Licha ya ulemavu wa mguu ameudhihirisha umma kwamba hauwezi kumfanya mtu kuwa tegemezi au ombaomba.

Kwa mara ya kwanza Mwananchi lilimkuta shambani kwake akiwa amesimama kwa mguu wa kushoto akipalilia nyanya alizolima kando ya barabara kuu ya Tanzania-Zambia eneo la Iwambi jijini humo.

Ingawa anatumia magongo kutembea, lakini awapo shamba hutumia mguu wa kushoto muda wote akisaidiwa na mpini wa jembe analotumia kulimia kupata uwiano unaomwezesha kusimama.

Alivyopata ulemavu

Kayuni anasema Januari 8, 1994 alipigwa risasi na mlinzi wa shamba moja eneo la Iwambi alipokuwa na wenzake wakifukua mabomba ya maji ili kwenda kuyaunganisha sehemu nyingine isiyo na maji.

Anasema mtaa wao ulikuwa na uhaba wa maji, hivyo wananchi chini ya mwenyekiti wao walikubaliana kuwa kwa vile eneo hilo kulikuwa na shamba la mifugo kulikuwa na mabomba yaliyowekwa na aliowataja kuwa Wachina, lakini yalikuwa hayatumiki hivyo wakakubaliana wakayafukue ili wayaunganishe eneo lenye maji na wayaelekeze mtaani kwao.

Anasema walipokuwa wakifanya kazi hiyo alifika mlinzi aliyefyatua risasi akiamini watu hao ni wavamizi ndipo moja ikatua mguuni kwake.

Kayuni anasema baada ya kuumia, siku iliyofuata uongozi wa shamba ulimchukua na kumpeleka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu zaidi ambako alikaa kwa miezi sita akitibiwa.

Kukatwa mguu

Anasema baada ya kufikishwa hospitalini hapo alifanyiwa upasuaji wa mguu na baadaye madaktari wakaufunga, lakini bahati mbaya sumu ilikuwa haijatoka yote mwilini jambo lililosababisha uanze kuoza.

Anasema Februari 8, 1994 ilibidi madaktari waamuru tiba pekee iliyokuwapo ni kuukata mguu huo.

Maisha baada ya kukatwa mguu

Kayuni anasema aliporejea nyumbani akawa ni mtu wa kukaa tu bila kazi yoyote ya kumuingizia kipato na kumtegemea mkewe ambaye naye hakuwa na kazi.

Anasema baada ya mguu kuimarika alianza biashara ya duka dogo la kuuza mahitaji ya nyumbani - biashara ambayo aliifanya kwa mwaka mmoja, lakini akaona haimudu, akaamua kuibadili.

Alianza kununua vitunguu swaumu vya jumla kutoka Mbeya na kuvipeleka Lusaka-Zambia - biashara ambayo aliifanya kwa mwaka mmoja, lakini nayo akaona ni ngumu kutokana na changamoto alizokuwa anakumbana nazo zilizotokana na ulemavu wake.

“Biashara hiyo nayo ilinishinda kutokana na kuwa na mikikimiki mingi, hivyo nikaamua kurejea kwenye kilimo ambacho ni asili yangu na tangu mwaka 1997 niliporejea hadi leo naendesha maisha yangu kwa kilimo,” anasema.

Kayuni anasema licha ya baba yake na ndugu zake waliopo nyumbani Ileje kuwa tayari kumsaidia hakuwa tayari kuukubali msaada huo na badala yake aliamini ana uwezo, afya njema na nguvu za kufanya kazi na kujitegemea.

“Tunaambiwa ‘mtegemea cha nduguye hufa maskini’ niliahidi nitakomaa mimi mwenyewe katika maisha yangu na ndiyo maana hadi leo hii nipo shambani hapa.”

Kilio chake

Kayuni anasema kwa sasa anafanya shughuli za kilimo kwenye eneo la robo ekari alilovamia ambalo ni mali ya Wakala wa Barabara (Tanroads), lililopo ndani ya hifadhi ya barabara ya Tanzam, Iwambi.

Anasema miaka yote amekuwa akilima eneo hilo, lakini anajua wakati wowote eneo hilo litachukuliwa na Serikali, hivyo anawaomba Watanzania na Serikali kumsaidia kupata ardhi ili aweze kuendesha maisha yake kupitia kilimo.



Chanzo: mwananchi.co.tz