Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Ombaomba Dar katika mtihani mzito

VIDEO: Ombaomba Dar katika mtihani mzito

Sat, 29 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Utembeapo katika barabara za katikati ya jiji la Dar es Salaam, si ajabu kukutana na watu wanaoomba fedha maarufu kama ‘ombaomba’.

Miongoni mwao wapo watu wenye ulemavu ambao wanaonekana kweli kuhitaji msaada, lakini pia wao waliokamilika viungo na siha njema.

Kwa muda mrefu uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam umeipiga vita uwepo wao na kufikia hatua ya kutenga maeneo kwa ajili ya watu wenye walemavu ili wafanye biashara na kuacha kuomba.

Pamoja na juhudi hizo wameendelea kuonekana katika maeneo ya katikati ya jiji wakiendelea na shughuli hiyo.

Hivi karibuni Manispaa ya Ilala ilipitisha sheria ya adhabu kwa watu watakaokutwa wakiwapatia fedha ombaomba ili kukomesha tabia hiyo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo atakayekutwa akimpa hela ombaomba atatozwa faini ya Sh200,000 ya hapo hapo, akishindwa kulipa atapelekwa mahakamani na faini yake ni Sh300,000 au kifungo cha miezi 12.

Pia Soma

Advertisement
Mkurugenzi wa halmashauri ya Ilala, Jumanne Shauri alisema wameamua kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanikisha kazi ya kuwaondoa ombaomba na barabarani na kuanzia sasa polisi watakuwapo kwenye makutano ya barabara za jiji, ili kuwakamata pamoja na watu watakaowapatia fedha au vitu.

Alisema sheria hiyo imekuja baada ya kuona hatua za kuwakamata na kuwatoza faini za Sh50,000 haijafanikiwa, kwani walikuwa wakilipa na kurudi barabarani.

“Ilala ni kitovu cha jiji na kumekuwa na malalamiko ya hawa ombaomba kujihusisha na udokozi kwenye magari, ndiyo maana tumeamua kushirikina na Polisi kukabiliana na tatizo hili,” alisema Shauri

Kuhusu wanaotaka kusaidia maskini, Shauri alieleza misaada ipelekwe kanisani, misikiti au kwenye makazi ya watoto yaliyopo Msongola na Vingunguti.

Mwananchi ilitembelea mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kushuhudia ombaomba hao wakiendelea na shughuli zao, huku wengine wakiwa na watoto wadogo.

Katika mataa ya kuelekea daraja la Salender na Kinondoni, walionekana wanawake wakiwa wameambatana na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitatu wakiomba kwenye magari.

Neema Samson, mmoja wa ombaomba alidai ana wiki moja tangu aje Dar es Salaam akitokea Dodoma.

Alisema amekuja kuomba baada ya kuona wenzake wamepata mafanikio kupitia shughuli hiyo, hivyo naye amekuja kujaribu bahati yake.

Kuhusu katazo la halmashauri ya Ilala, Neema alisema halina nia njema kwao na linalenga kuwadidimiza kwenye umaskini uliokithiri.

“Wanapozuia watu wenye nia njema kutusaidia ni kama wanataka tufe kwa njaa, hiki wanachofanya si sahihi, kama ni hivyo basi Serikali iangalie inatusaidia vipi kuondoka kwenye hali ngumu,” alisema Neema.

Kilio kama hicho kilitolewa na Paul Robi ambaye ni mlemavu aliyeeleza wakati mwingine analazimika kuomba ili apate fedha za kujikimu.

Tofauti na ombaomba wengine, Robi alikiri kuwa na eneo la kufanya biashara ndogo ndogo ila anapoona mambo magumu huingia barabarani kuomba.

“Nina biashara lakini mambo yanapokuwa magumu nakuja huku barabarani na nashukuru Mungu huwa napata kuanzia Sh10,000 hadi Sh100,000,” alisema Robi

Kwa upande wake, Hawa Hamis alisema, “watu kama sisi wenye ulemavu huwa tunanyayapaliwa na hata nikipika maandazi hakuna mtu atakayenunua, ndio maana nakaa barabarani kuomba ili nipate hela ya kusomesha watoto wangu.

“Kuzuia watu wasitusaidia ni kuzidi kutukandamiza. Hatupendi kukaa kuomba, bali hali ya maisha ni ngumu.”

Akizungumzia hilo, kaimu meya wa jiji la Dar es Salaam, Abdala Mtinika alisema ili ombaomba waondoke ni lazima watu waache kuwapatia fedha na kuwashauri kutafuta shughuli halali ya kufanya.

“Kwa mazingira ya nchi yetu si sahihi kuwa na ombaomba, tuna ardhi yenye rutuba, viwanda ambavyo vinahitaji rasilimali watu inakuwaje mtu mwenye viungo vyote asimame barabarani kuomba?

“Hata kwa wale wenye ulemavu sasa hivi kwenye halmashauri kuna fedha zimetengwa kwa ajili yao ili wafanye biashara ndogondogo na ikishindikana Serikali inasaidia kaya maskini kupitia Tasaf. Warudi kwenye maeneo yao watasaidiwa huko kwa utaratibu maalum,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz